Waafrika Kusini wapinga azma ya Shell kuchimba mafuta pwani ya nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i77694-waafrika_kusini_wapinga_azma_ya_shell_kuchimba_mafuta_pwani_ya_nchi_hiyo
Wananchi wa Afrika Kusini wamefanya maandamano katika fukwe za nchi hiyo kupinga mpango wa shirika la mafuta la Uingereza na Uholanzi la Royal Dutch Shell wa kuchimba mafuta katika pwani ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2021 23:46 UTC
  • Waafrika Kusini wapinga azma ya Shell kuchimba mafuta pwani ya nchi hiyo

Wananchi wa Afrika Kusini wamefanya maandamano katika fukwe za nchi hiyo kupinga mpango wa shirika la mafuta la Uingereza na Uholanzi la Royal Dutch Shell wa kuchimba mafuta katika pwani ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Katika maandamano hayo yaliyofanyika jana Jumapili, waandamanaji walisikika wakipiga nara za kupinga mpango huo, wakisisitiza kuwa uchimbaji huo wa mafuta utaleta uharibifu wa mazingira na kutishia maisha ya wanyama wa baharini kama papa, pomboo na nyangumi. 

Mmoja wa waandamanaji hao katika mji bandari wa Port Edward ulioko kusini mwa pwani ya Kwazulu Natal, Kas Wilson ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "inaogofya hata kutakafari tu wataruhusiwa kulifanya hili.... jambo hili halikubaliki, tutalisimamisha."

Wananchi wa Afrika Kusini wamesema hawataruhusu uchimbaji huo wa mafuta ufanyike katika eneo la Wild Coast, kwani ukanda huo ambayo ni sehemu ya pwani ya mkoa wa Eastern Cape nchini humo, mbali na kuwa na mandhari mazuri ya kuvutia na vituo vingi vya utalii, lakini pia ni eneo linalohifadhi spishi nyingi za wanyama hususan wa baharini.

Ijumaa iliyopita, mahakama moja nchini Afrika Kusini ilikataa ombi la wanamazingira wa nchi hiyo la kutaka uchimbaji huo mkubwa wa mafuta usimamishwe, ikidai kuwa upande uliowasilisha faili mahakamani haujatoa ushahidi wa kuthibitisha kuwa mradio huo utakuwa na taathira hasi kwa mazingira.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, shirika la Shell ambalo linaongoza katika uzalishaji mafuta ghafi ya petroli nchini Nigeria linakabiliwa na kesi kadhaa mahakamani kutokana na kuhusika kwake katika ukandamizaji uliopelekea kunyongwa mtetezi wa haki katika eneo la Ogoniland, Ken Saro-Wiwa na wenzake wanane waliohukumiwa kifo mwaka 1995.