Jeshi la Kenya laangamiza al-Shabaab 21 nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7810-jeshi_la_kenya_laangamiza_al_shabaab_21_nchini_somalia
Jeshi la Ulinzi la Kenya KDF limetangaza habari ya kuangamizwa wanachama 21 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika eneo la Hawina nchini Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 25, 2016 10:03 UTC
  • Jeshi la Kenya laangamiza al-Shabaab 21 nchini Somalia

Jeshi la Ulinzi la Kenya KDF limetangaza habari ya kuangamizwa wanachama 21 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika eneo la Hawina nchini Somalia.

Msemaji wa KDF, Kanali David Obonyo amethibitisha habari hizo za kuuawa wanamgambo wa al-Shabaab akiwemo Salad Bart, kamanda wa ngazi ya chini wa kundi hilo.

Amesema kundi hilo lilijaribu kuuzingira msafara wa magari ya jeshi hilo uliokua ukielekea Tabda kutoka Dobley katika barabara ya Tabda na hapo ndipo makabiliano yakaanza.

Msemaji wa Jeshi la Kenya amesema hakuna askari yeyote wa KDF aliyejeruhiwa au kuuawa katika makabiliano hayo. Kadhalika KDF imekamata bunduki 17 aina ya AK-47, maroketi, maguruneti pamoja na silaha nyingine baada ya kupambana na magaidi hao hayo.

Somalia imekuwa ikishuhudia machafuko tangu mwaka 2006, baada ya kundi la kigaidi la al-Shabaab kuanzisha harakati zake kufuatia kukosekana serikali kuu yenye nguvu nchini humo.

Hii ni katika hali ambayo, nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inatarajiwa kufanya uchaguzi wa rais mwezi Agosti mwaka huu.