Libya yamtaja balozi wa Uingereza kuwa hatakikani nchini humo
Bunge la Libya limemtaja balozi wa Uingereza nchini humo kuwa ni mtu asiyetakikana nchini humo. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya matamshi yaliyotolewa na balozi wa Uingereza yaliyotambuliwa kuwa yamekiuka sheria za kimataifa.
Msemaji wa Baraza la Wawakilishi la Libya, Abdullah Belhaq amesema: "Matamshi ya balozi wa Uingereza, Caroline Hurndall, ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na uhuru wa Libya."
Awali balozi huyo alikuwa amesema kuwa, London inaitambua rasmi Serikali ya Umoja wa Kitaifa tu hadi pale uchaguzi utakapofanyika, na inapinga kuundwa kwa serikali na taasisi kinzani.
zikiendelea kuingilia masuala ya ndani ya Libya, Marekani, Uingereza, Ujerumani, Italia na Ufaransa zimetaka kuainishwa haraka tarehe ya mwisho ya kuitishwa uchaguzi nchini Libya.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na nchi hizo tano Ijumaa jioni, ilitishia kuwawekea vikwazo wale wote wanaoghushi au kuhujumu mchakato wa uchaguzi wa Libya.
Mapema mwezi huu Baraza Kuu la Serikali ya Libya lilipendekeza kuwa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo ufanyike mwezi Februari mwakani sawa na ule wa Bunge badala ya tarehe 24 Disemba mwaka huu.
Naibu Mkuu wa Baraza Kuu la Uongozi Libya, Omar Abdel Aziz Bushah alisema mchakato wa sasa wa uchaguzi unaweza kucheleweshwa kutokana na masuala mbalimbali yanayoitatiza Tume Kuu ya Taifa ya Uchaguzi.
Kurejea kwa Saiful Islam Gaddafi katika kinyang'anyiro cha urais, kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Sabha (kusini mwa Libya), kumechanganya tena karata nchini Libya, hasa kutokana na kukithiri kwa mizozo na mivutano kati yake na Jenerali mstaafu, Khalifa Haftar katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
Khalifa Haftar na Saiful Islam Gaddafi wanasakwa na Hahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa tuhuma za kutenda uhalifu wa kivita