Mjadala kuhusu mswada katika bunge la Kenya waibua mapigano
Kikao cha Bunge la Kenya kimebadilika na kuwa ulingo wa ndondi baada ya wabunge kadhaa kuanza kupigana wakati mjadala ukiendelea kuhusu muswada wa muungano ulioibua mgawanyiko.
Wabunge kadhaa wa Kenya walielekea mahali anapoketi Spika na kuanza kurushiana vijembe huku wabunge wengine wakiwarushia wenzao chupa za maji katika tukio hilo lililoibua purukushani bungeni.
Ghasia ziliibuka wakati wabunge walipokuwa wakipiga kura kuhusu mabadliko yaliyopendekezwa na mbunge wa Kandara, Alice Wahome, kwa lengo la kuondoa kifungu kuhusu kuanzisha muungano wa vyama. Mbunge Alice Wahome alipinga kwa kusema kuwa kifungu cha 6 cha muswada uliopendekezwa ni kinyume na Katiba na kwamba kinapaswa kuondolewa. Amesema suala la kuja na muungano wa kisiasa ni kinyume na Katiba.

Kifungu cha 6 cha muswada huo pamoja na mambo mengine, kinaeleza bayana kuhusu utaratibu unaopaswa kufuatwa katika kusajili chama cha siasa. Kifungau hicho pia kinaeleza kuwa, uongozi wa chama cha muungano utakuwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazohusiana na utawala wa muungano wa vyama.
Kipengee cha Katiba kinabainisha kuwa mwanachama wa muungano fulani hatakuwa mwachama wa muungano mwingine.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, vyama vya Uhuru na Odinga vinataka kubadili sheria ili kuviwezesha vyama hivyo kujiunga na harakati ya Azimio la Umoja bila ya kupoteza utambulisho wao.