Algeria yaufungua tena ubalozi mdogo nchini Libya
Algeria imefungua tena ubalozi wake mdogo huko Tripoli mji mkuu wa Libya baada ya kufungwa kwa miaka minane.
Shirika la habari la Iran, IRNA limeripoti kuwa, ubalozi huo mdogo wa Algeria umefunguliwa katika sherehe iliyyohudhuriwa na balozi Suleiman Shanin, na Issa Ramani balozi wa Algeria huko Libya na wawakilishi wa wananchi wa Algeria wanaoishi Libya.
Viongozi wa Algeria wamesisitiza kuwa, ubalozi mdogo wa nchi hiyo umefunguliwa Libya katika fremu ya kuwalinda wahajiri wanaoishi nje ya nchi na pia kwa lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya wmataifa hayo mawili; nchi ambazo pia zina mpaka mrefu wa pamoja.
Mwezi Mei mwaka 2014 Algeria iliwaondoa haraka wafanyakazi wa ubalozi wake nchini Libya na kufunga vituo vyake vya kidiplomasia baada ya kupata taarifa kwamba, makundi ya kigaidi yanajaribu kuishambulia Libya.
Wakati huo, Waalgeria zaidi ya elfu tatu walikwama Libya kutokana na kumalizika muda wa pasi zao za kusafiria huku wengine wakitaabika kimya kimya.
Serikali ya Algeria mwishoni mwa mwaka jana ilimrejesha Tripoli balozi wake, Suleimani Shanin.