Maiga: Ufaransa, chimbuko la matatizo yote ya kiusalama, kiuchumi Mali
Waziri Mkuu wa Mali amesema Ufaransa ndiyo sababu ya matatizo mbalimbali ya kiusalama na kiuchumi yanaoisumbua nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Choguel Kokalla Maiga amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Anadolu la Uturuki na kuongeza kuwa, Ufaransa imekuwa na ushawishi mkubwa katika kuathiri maamuzi yanayofanywa na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) dhidi ya Mali.
Amesema ni jambo la kusikitisha kuwa Ufaransa huwa na taarifa za ajenda zitakazojadiliwa na matokeo ya mikutano ya ECOWAS, hata kuliko baadhi ya viongozi wa jumuiya hiyo ya kieneo.
Waziri Mkuu wa Mali ametoa mfano wa vikwazo vilivyotangazwa na Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi Januari 9 dhidi ya Mali, na kueleza kuwa mamlaka ya Ufaransa zilikuwa zimegusia kuhusu uwezekano wa kuwekewa vikwazo nchi hiyo mwezi mmoja kabla.
Haya yanaripotiwa huku maelfu ya wananchi wa Mali wakijitokeza katika maandamano makubwa dhidi ya Ufaransa katika mji mkuu wa nchi hiyo Bamako, huku wakisherehekea kutimuliwa balozi wa Ufaransa nchini humo. Waandamanaji walikusanyika katikati ya Bamako wakiwa na bendera za Mali huku wakiteketeza moto picha za Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.
Mali ilimtimua balozi wa Ufaransa siku chache zilizopita, kutokana na matamshi yaliyojaa chuki na uhasama ya viongozi wa dola hilo ambalo liliikoloni Mali na nchi zingine za Afrika.