Sisitizo la Ufaransa la kuendelea kuwepo eneo la Sahel
Pamoja na kushuhudiwa mivutano hivi karibuni kati ya Ufaransa na baadhi ya nchi za eneo la Sahel barani Afrika ikiwemo Mali, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa Jean Yves Le Drian amesisitiza kuwa Ufaransa haitatoka katika eneo la Sahel hata kama itaondoa wanajeshi wake kikamilifu huko Mali.
Hali ya mvutano imeshuhudiwa katika miezi ya karibuni baina ya Mali na Ufaransa na hali hiyo imepamba moto baada ya kujiri mapinduzi mwaka 2021 huko Mali. Ni wazi kuwa baada ya kujiri mapinduzi huko Mali na kuchukua madaraka Kanali Assimi Goita uhusiano wa Bamako na Paris umekumbwa na mivutano na hitilafu nyingi kuhusiana na suala zima la kuwepo kijeshi Ufaransa nchini humo. Baraza la Kijeshi linaloongoza Mali limetangaza kuwa halitambui tena makubaliano ya kiulinzi yaliyofikiwa kati ya nchi hiyo na Ufaransa na kwamba halitatekeleza makubaliano hayo tajwa. Baraza hilo aidha karibu mwezi mmoja uliopita lilimfukuza balozi wa Ufaransa huko Mali.
Duru mpya ya mivutano kati ya Ufaransa na Mali ilianza kufuatia kufukuzwa balozi wa Ufaransa nchini humo. Hii ni katika hali ambayo, Ufaransa ilituma wanajeshi wake katika eneo la Sahel na khususan huko Mali tokea mwaka 2014 katika kile ilichokitaja kuwa kwa ajili ya kupambana na ugaidi; ambapo nchi hiyo ilituma wanajeshi wake karibu 4,500 katika fremu ya oparesheni ya Barkhane kwa lengo la kuyafurusha makundi ya kigaidi na wanamgambo wenye misimamo mikali wanaoendesha harakati zao katika nchi jirani na Mali. Nchi za eneo la Sahel khususan Mali hairidhishwi na inapinga kuwepo kijeshi Ufaransa na uingiliaji unaofanywa na Paris katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Kwa mtazamo wa Mali, Ufaransa na waitifaki wake wanajaribu kila linalowezekana kuendeleza siasa zao za kikoloni katika kalibu ya ukoloni mamboleo badala ya kuendesha vita dhidi ya makundi ya kigaidi.
Choguel Kokalla Maiga Waziri Mkuu wa Mali amesema kuwa serikali ya sasa ya nchi hiyo imejifunza kutokana na historia kwa kuzingatia matukio yaliyoshuhudiwa duniani katika kipindi cha miaka 20 au 30 iliyopita. Amesema serikali ya Mali imebaini hali hiyo na inafahamu vyema kuwa Paris ingali na lengo la kulidhibiti bara la Afrika. Waziri Mkuu wa Mali amesisitiza kuwa makundi yanayotaka kujitenga yalikimbilia katika eneo la Sahel yakitokea Tripoli kwa uungaji mkono wa Ufaransa baada ya kupinduliwa Muammar Gaddafi huko Libya mwaka 2011. Hii ni kwa sababu makundi hayo hadi sasa bado yanauungwa mkono moja kwa moja na Paris yakipatiwa silaha na zana za kijeshi; na ni dhahir shahir kuwa Paris imeyaahidi makundi hayo kuwa itaikalia kwa mabavu Mali, italigawa eneo la kaskazini mwa Mali na kuasisi nchi huru.
Mali ni moja ya nukta muhimu kwa Ufaransa barani Afrika. Nchi hiyo ina maliasili nyingi za mafuta na gesi, urani na dhahabu; na Ufaransa ni miongoni mwa nchi zilizo na haki ya kuchimba mafuta nchini humo. Ufaransa pia ni nchi inayotumia pakubwa urani kutoka Mali. Kwa msingi huo, lengo la Paris katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita limekuwa ni kulinda maslahi yake ya kifedha na kunufaika kibishara na kiuchumi huko Mali licha ya madai mengine yote ya kidhahiri yanayotolewa na nch hiyo ya Magharibi kuhusu bara la Afrika.
Kuendelea harakati za makundi ya kigaidi huko Mali, katika eneo la Sahel na mauaji yanayofanywa na makundi hayo ni ushahidi wa wazi wa kufeli madai ya Paris katika kupambana na ugaidi. Choguel Maiga Waziri Mkuu wa Mali amewataja wanajeshi wa Ufaransa kuwa ni mamluki wanaofanya mazoezi ya kijeshi katika ardhi ya Mali katika kalibu ya vikosi vya jeshi. Hii ni katika hali ambayo, kabla ya hapo Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya Mali alizungumzia suala hilo akisema: Upo ushahidi unaoonyesha kuwa wanajeshi wa Ufaransa waliowasili huko Mali kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi wanatoa mafunzo kwa makundi hayo.
Mivutano inayoendelea sasa imewapelekea viongozi wa Paris kutangaza kuwa eti wataondoa wanajeshi wao huko Mali licha ya kuwa wataendelea kupambana na makundi ya kigaidi katika nchi jirani. Kuhusiana na hilo Jean Yves Le Drian Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa amesema, iwapo mazingira hayataandaliwa na kuwawezesha kuchukua hatua huko Mali basi wataendelea kushirikiana na nchi nyingine za eneo la Sahel katika vita dhidi ya ugaidi ambazo zimetaka uwepo kamili wa wanajeshi wa Ufaransa.
Inaonekana kuwa licha ya madai yote hayo ya Ufaransa, nchi hiyo si tu haiko tayari kuondoka katika nchi za Sahel bali inatumia nyenzo mbalimbali kuendeleza sera zake za kikoloni. Si Mali tu bali hata nchi nyingine za Kiafrika pia haziko tayari kuafiki tena sera za uwongo za nchi hiyo yeye kupora maliasili za nchi za Kiafrika.
Ismail Bukanan, mhadhiri wa masuala ya siasa katika Chuo Kikuu cha Rwanda anasema: Ufaransa inapasa kubadili stratejia yake barani Afrika.