Ufaransa na washirika wake sasa kuondoa majeshi yao vamizi nchini Mali
Ufaransa na washirika wake wametangaza kuwa, wataondoa askari wao wote kutoka katika nchi ya Mali iliyoko magharibi mwa Afrika.
Askari hao wa kigeni wa Ufaransa na washirikak wake wanatarajiwa kuondoka nchini Mali baada ya kuweko katika nchi hiyo kwa muongo mmoja.
Mivutano baina ya Ufaransa na Mali imeongezeka mno katika miezi ya hivi karibuni hasa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka jana (2021).
Baada ya uhusiano wa Ufaransa na Mali kuharibika, viongozi wa Ulaya wametangaza katika taarifa yao ya pamoja leo kwamba, Ufaransa na washirikak wake wanaondoka askari wao wote katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika baada ya kuweko huko kwa muongo mmoja.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Waziri wa UIinzi wa Ufaransa alizungumzia uwezekano wa kuondoka majeshi ya Ufaransa katika nchi ya Mali ambayo imekuwa ikikodolewa macho ya tamaa na madola ya kibeberu kutokana na kuwa na madini ya dhahabu na urani.
Ufaransa, Canada na mataifa mengine yenye askari huko Mali yamedai katika taarifa yao kwamba, yamechukua uamuzi huo kutokana na vizingiti vinavyowekwa na viongozi wa Bamako.
Mapema mwezi huu Waziri Mkuu wa Mali, Choguel Kokalla Maiga, aliishutumu serikali ya kikoloni ya Ufaransa kwa vitendo vyake dhidi ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na kusema kuwa, Wafaransa walipaswa kuisaidia Mali, lakini badala yake wanayasaidia magenge ya kigaidi yanayopigania kujitenga na wanazichochea nchi za Ulaya ziliwekee vikwazo taifa hilo la Kiafrika.