Turathi zilizoibiwa na mkoloni Muingereza zarejeshwa Nigeria baada ya karne
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i80558-turathi_zilizoibiwa_na_mkoloni_muingereza_zarejeshwa_nigeria_baada_ya_karne
Turathi mbili muhimu za kihistoria za Nigeria zilizoibiwa na Uingereza katika enzi za ukoloni hatimaye zimerejeshwa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, baada ya kupita zaidi ya miaka mia moja.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 20, 2022 04:26 UTC
  • Turathi zilizoibiwa na mkoloni Muingereza zarejeshwa Nigeria baada ya karne

Turathi mbili muhimu za kihistoria za Nigeria zilizoibiwa na Uingereza katika enzi za ukoloni hatimaye zimerejeshwa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, baada ya kupita zaidi ya miaka mia moja.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, shaba mbili nyeusi zilirejeshwa jana Jumamosi katika kasri la kitamaduni katika kijiji Benin, ambayo makao makuu ya jimbo la Edo, kusini mwa Nigeria. 

Athari hizo za kihistoria ziliibiwa na wanajeshi wa Uingereza wakati nchi hiyo ya Ulaya ilikuwa imeikoloni Nigeria, kuanzia katikati ya karne ya 19, hadi mwaka 1960.

Hatua ya kurejeshwa turathi na athari hizo za kihistoria nchini Nigeria imefungua tena mjadala mkubwa wa kidiplomasia kuhusu dafina na vitu vya kale vya thamani vilivyoporwa na wakoloni barani Afrika.

Ramani ya Nigeria

Weledi wa mambo wanatumai kuwa, maelfu ya turathi za kihistoria zilizoibiwa wa wakoloni barani Afrika katika enzi za ukoloni zitarejeshwa katika nchi zao za asili.

Mbali na Uingereza, Ufaransa pia ilichukua turathi baina ya 4500 na 6000 za Benin katika vita vya mwaka wa 1892 hadi 1894, huku wamishonari wa Kikristo wa nchi hiyo pia wakipora vitu vya thamani vya raia walivyovitambua kuwa ni hirizi.

Nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikitaka kurejeshwa turathi na dafina zao za kale zilizoporwa na wakoloni wa Ulaya wakati wa kipindi cha ukoloni.