Umoja wa Mataifa kupatanisha Libya baada ya serikali hasimu kuapishwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81046-umoja_wa_mataifa_kupatanisha_libya_baada_ya_serikali_hasimu_kuapishwa
Umoja wa Mataifa umetangaza utayarifu wa kupatanisha mgogoro wa kisiasa nchini Libya baada ya kuibuka serikali mbili hasimu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 05, 2022 14:11 UTC
  • Umoja wa Mataifa kupatanisha Libya baada ya serikali hasimu kuapishwa

Umoja wa Mataifa umetangaza utayarifu wa kupatanisha mgogoro wa kisiasa nchini Libya baada ya kuibuka serikali mbili hasimu.

Stepanie Williams Mshauri Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Libya ametoa kauli hiyo baada ya Bunge Libya lenye makao yake mashariki mwa nchi kumuapisha Fat'hi Bashagha katika kile kinachoonekana ni kukabiliana ana kwa ana na Waziri Mkuu wa sasa Abdul Hamid Dbeibah. Hatua hiyo imezusha wasiwasi wa kuibuka mgogoro mpya wa kisiasa nchini Libya.

Williams ameandika katika ukurasa wake wa Tiwtter kuwa suluhusho la Libya haliko katika kuunda serikali mbili hasimu na kuwepo kipindi cha mpito kisicho na kikomo.

Amesema, ametoa wito kwa Bunge la Baraza la Wawakilishi lenye makao yake mjini Tobruk na Bunge la Seneti lenye makao yake Tripoli kuunda kamati ya wajumbe sita kila upande ili kujadili mwafaka wa katiba. Amependekeza kuwa kamati hiyo ikutane Machi 15 chini ya Umoja wa Mataifa ili kujadili mchakato wa uchaguzi.

Baraza la Wawakilishi Libya linasema muhula wa Dbeibah ulimalizika Disemba 24 wakati uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika ulipoakhirishwa. Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Libyya Dbeibah anasema hataondoka madarakani na hawezi kukabidhi madaraka isipokuwa tu kwa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wenyewe wa Libya.