Arab League yaelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya kisiasa nchini Libya
-
Ahmed Aboul Gheit
Kuongezeka kwa tofauti kati ya mirengo ya Libya kuhusu utungaji wa sheria za uchaguzi wa rais na wabunge kumekuwa tishio kubwa kwa mchakato wa uchaguzi, kwa kadiri kwamba Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit ameeleza wasiwasi wake juu ya hali ya kisiasa ya nchi hiyo na umuhimu wa kuwepo mwafaka na maridhiano ya kisiasa.
Kwa sasa hali ya kisiasa nchini Libya si shwari, na uchaguzi wa rais ambao ulikuwa umepangwa kufanyika Disemba 24, umeahirishwa kwa sababu mbalimbali. Miongoni mwa sababu hizo ni ukosefu wa maelewano kati ya makundi ya Libya kuhusu suala la kutungwa sheria ya uchaguzi na matatizo ya mahakama yanayotokana na malalamiko dhidi ya baadhi ya wagombea wa uchaguzi wa rais. Matatizo hayo yameongezeka zaidi katika miezi ya hivi karibuni, na inahofiwa kuwa yanaweza kuvuruga zaidi mchakato wa kurejesha amani na utulivu nchini Libya. Ni kwa kuzingatia hali hiyo, ndiyo maana Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu akaeleza wasiwasi wake kuhusu yanayojiri nchini Libya.
Miongoni mwa matatizo ya sasa ya Libya ni hitilafu na mivutano kuhusu utungaji wa sheria na nafasi mbalimbali za uongozi. Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abdul-Hamid Dbeibah ambaye alichukua madaraka mwaka jana kupitia mchakato ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa, anasema hataondoka madarakani na hatakabidhi madaraka isipokuwa kwa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wenyewe wa Libya. Ni baada ya Bunge Libya lenye makao yake Mashariki mwa nchi kumchagua kwa sauti moja Fat'hi Bashagha kuwa waziri mkuu wa serikali mpya katika kile kinachoonekana ni kukabiliana ana kwa ana na Waziri Mkuu wa sasa, Abdul Hamid Dbeibah. Baraza la Wawakilishi la Libya linasema muhula wa Dbeibah ulimalizika Disemba 24. Suala hilo limezidisha tofauti na kuvuruga mchakato wa kutunga sheria za uchaguzi wa rais na wabunge nchini Libya.
Kwa upande mwingine, Bunge la Libya likiongozwa na Aguila Saleh Issa limetunga sheria za uchaguzi, lakini Baraza Kuu la Libya, chini ya uenyekiti wa Khalid al-Mishri, limezikataa sheria hizo na kutangaza kuwa, zimepitishwa bila ya idhini ya Baraza Kuu.
Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Stephanie Williams, anasisitiza umuhimu wa kulindwa usalama na utulivu na kuzuia vitendo vyovyote vya unyanyasaji, vitisho, utekaji nyara, uchochezi na ghasia na kusema: Utatuzi wa mgogoro wa Libya hauko katika uundaji wa serikali hasimu na kutangzwa awamu endelevu za mpito, bali ni mchakato wa kuelekea kwenye makubaliano ambayo yanatoa kipaumbele kwa suala la kulindwa umoja na ardhi yote ya nchi hiyo.
Kwa sasa kuna wasiwasi mkubwa juu ya mgawanyiko na hitilafu kati ya makundi na mirengo tofauti ya Libya, na iwapo hali hiyo itaendelea, sio tu kwamba uchaguzi na uundaji wa serikali ya kidemokrasia utakabiliwa na vizingiti na hatari kubwa, lakini pia kuna hofu kwamba mchakato wa kurejesha amani utasimama na hatimaye Libya itatumbukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kisiasa, Rosemary DiCarlo ameashiria hitilafu za kimitazamo kuhusu uchaguzi na makabidhiano ya amani ya madaraka nchini Libya na kuonya kuwa: "Njia ya Libya kuelekea kwenye umoja na amani, ni tete na nyeti."
Pamoja na hayo yote inaonekana kuwa, njia pekee ya kuiokoa Libya na kutatua mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika ni kufikia mwafaka wa jinsi ya kufanya uchaguzi.