Ufaransa yakosolewa kwa kupiga mnada turathi yenye thamani ya Gabon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81846-ufaransa_yakosolewa_kwa_kupiga_mnada_turathi_yenye_thamani_ya_gabon
Ufaransa imepuuza malalamiko ya wananchi na maafisa wa Gabon, na kwa jeuri imepiga mnada barakoa ya kitamaduni ya nchi hiyo ya Kiafrika kwa yuro milioni 4.2.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 27, 2022 06:19 UTC
  • Ufaransa yakosolewa kwa kupiga mnada turathi yenye thamani ya Gabon

Ufaransa imepuuza malalamiko ya wananchi na maafisa wa Gabon, na kwa jeuri imepiga mnada barakoa ya kitamaduni ya nchi hiyo ya Kiafrika kwa yuro milioni 4.2.

Jana Jumamosi Ufaransa iliipiga mnada maski adimu ya “Ngil” iliyokuwa ikitumiwa na watu wa jamii ya Fanga nchini Gabon katika karne ya 19, licha ya wanaharakati wa Gabon kuandamana kulalamikia mauzo hayo kwenye ukumbi wa mnada.

Turathi hiyo ya kihistoria iliyouzwa katika mnada uliofanyika mjini Montpellier, kusini mwa Ufaransa, awali ilikiswa kuwa ingeliuzwa kwa thamani ya yuro 300,000-400,000, lakini ikaishia kuuzwa kwa yuro milioni 4.2.

Wagabon wamelaani kitendo hicho cha kupigwa mnada turathi hiyo ya kihistoria ya nchi yao, wakisisitiza kuwa Ufaransa imepokea bidhaa ya wizi inayopaswa kurejeshwa nchini kwao. Hiyo jana pia katika soko hilo la mnada nchini Ufaransa, 'Kiti cha Kongo' kiliuzwa kwa yuro 44,000.

Hatua ya kupigwa mnada turathi na athari hizo za kihistoria za Gabon na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini Ufaransa imefungua tena mjadala mkubwa kuhusu dafina na vitu vya kale vya thamani vilivyoporwa na wakoloni barani Afrika.

Ukoloni wa Ulaya barani Afrika

Ufaransa pia katika enzi za ukoloni iliiba turathi baina ya 4500 na 6000 za Benin katika vita vya mwaka wa 1892 hadi 1894, huku wamishonari wa Kikristo wa nchi hiyo pia wakipora vitu vya thamani vya raia walivyovitambua kuwa ni hirizi.

Nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikitaka kurejeshwa turathi na dafina zao za kale zilizoporwa na wakoloni wa Ulaya wakati wa kipindi cha ukoloni.