Jitihada za kumshawishi Al-Dbeibeh akabidhi madaraka Libya zaendelea
Waziri Mkuu mpya wa Libya Fathi Bashagha amesema jitihada zinafanywa za kumshawishi waziri mkuu wa serikali ya mpito Abdul Hamid al-Dbeibah akubali kung'atuka madarakani na kumkabidhi yeye hatamu za uongozi.
Tarehe 10 Februari, vyombo vya habari vya Libya vilitangaza kuwa, Fathi Bashagha, waziri wa zamani wa mambo ya ndani amechaguliwa kwa wingi mkubwa wa kura na bunge la nchi hiyo kuwa waziri mkuu mpya ili kuchukua nafasi ya waziri mkuu wa serikali ya mpito Abdul Hamid al-Dbeibah.
Kutokana na kutokuwepo umoja kati ya taasisi ya jeshi na nyadhifa za utawala, Libya imeshindwa kuwa na uthabiti na badala yake inashuhudia ombwe la kisiasa kutokana na tofauti za mitazamo baina ya mirengo ya ndani ya nchi hiyo.
Jamii ya kimataifa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya zimekuwa zikisisitiza kuwa njia pekee ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo ni kufanyika uchaguzi wa rais na bunge.
Kwa mujibu wa shirika la habari la ISNA, Waziri Mkuu wa Libya Fathi Bashagha ameongeza kuwa, juhudi hizo zimeanza kufanywa ili kumshawishi Dbeibah akubali kuachia hatamu za uongozi mkabala wa kudhaminiwa usalama wake na kupatiwa kinga ya kisiasa.
Siku ya Jumanne na baada ya masaa kadhaa, Bashagha alitangaza kuwa yuko tayari kuingia mji mkuu Tripoli, sambamba na kusisitiza zichukuliwe hatua za kuepusha kutokea mapigano na umwagaji damu katika mji mkuu huo wa Libya.../