Mahakama ya Rufaa Misri yapasisha kifungo cha maisha jela dhidi ya Badie
Mahakama ya Rufaa nchini Misri imepitisha hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa kiongozi wa chama cha Ikhwanul Muslimin (Muslim Brotherhood) Mohammed Badie.
Shirika la Habari la Iran, (IRNA) mapema leo asubuhi limeripoti kuwa, Mahakama ya Rufaa ya Misri jana Jumatano iliidhinisha hukumu ya kifungo cha maisha jela dhidi ya "Mohammad Badie", "Mohamed al-Beltagi " na "Safwat Hegazi", viongozi wa Ikhwanul Muslimin ya Misri.
Hukumu hizo zinahusiana na kesi ya ghasia katika jimbo la Port Said mwaka 2013, ambapo watu watano waliuawa. Mwaka 2015 Mahakama ya Jinai ya Misri ilimtia hatiani kiongozi huyo wa Ikhwanul Muslimin na wenzake 66 kwa tuhuma za kuhusika na ghasia hiizo. Hata hivyo, chama cha Muslim Brotherhood hakikukubali shutuma hizo dhidi ya wanachama wake na kilipinga hukumu hiyo.
Jumapili iliyopita pia Mahakama ya Misri imemhukumu kifungo cha maisha jela kiongozi wa muda wa Ikhwanul Muslimin katika kesi inayojulikana kwa jina "kujipenyeza katika mipaka ya Mashariki".
Awali vyombo vya habari vya Misri vilikuwa vimeripoti kuwa, Idara ya Mahakama ya nchi hiyo imeidhinisha hukumu ya kifo dhidi ya Mahmoud Ezzat Ibrahim, kiongozi wa muda wa Ikhwanul Muslimin kwa kuhusishwa na faili la tuhuma za kushirikiana na makundi ya kigeni dhidi ya maslahi ya taifa hilo.
Kesi hiyo inahusishwa na matukio ya mwaka wa 2011 ambapo watu kadhaa, wakiwemo wanachama wa Ikhwanul Muslimin, walituhumiwa kuvamia gereza la Wadi El Natrun na kushambulia vituo kadhaa vya usalama vya Misri.
Mahmoud Ezzat ni mmoja kati ya watu muhimu wa katika harakati ya Ikhwanul Muslimin na anajulikana kama "mlinzi wa mali na siri za kundi hilo".
Kufuatia kukamatwa kwa Mohammad Badie mwaka 2013, harakati hiyo ilimtangaza Mahmoud Ezzat kuwa kiongozi wa muda wa kundi hilo.
Serikali ya Misri inakitambua chama cha Ikhwanul Muslimin (Muslim Brotherhood) kama "kundi la kigaidi" na ilipiga marufuku shughuli zote za chama hicho baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoindoa madarakani serikali ya Mohamed Morsi. Mapinduzi hayo yaliongozwa na kiongozi wa sasa wa nchi hiyo Jenerali Abdel Fattah al Sisi.