Kiongozi wa DAESH (ISIS) mwenye ushawishi mkubwa Burkina Faso aangamizwa na jeshi
Jeshi la Burkina Faso limetangaza kuwa limewaua magaidi kumi na wawili, akiwemo Tidiane Djbrilou Dicko, kiongozi wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) katika eneo la Sahara Kuu.
Duru za makao makuu ya jeshi la Burkina Faso zimeeleza kuwa, Dicko aliangamizwa katika operesheni ya mashambulio ya anga iliyofanywa Alkhamisi, Mei 26 katika wilaya ya Tongomayel, mkoani Soum.
Kulingana na vyanzo kadhaa vya usalama, Tidiane Djibrilou Dicko anatambulika ndani ya Burkina Faso kuwa mtu katili akiwa na wafuasi miongoni mwa vijana wengi katika jimbo la Soum. Ukatili wake ulidhihirika baada ya shambulio la kigaidi dhidi ya kijiji alikozaliwa cha Silgadji.

Shambulio hilo la Januari 2020 liliteketeza roho za takriban watu arubaini. Tidiane Djibrilou na wapiganaji wake walizingira watu kwenye soko la kijiji hicho ambapo wanaume waliuawa na wanawake waliamriwa kuondoka.
Kwa mujibu wa afisa mkuu wa jeshi la Burkina Faso, Dicko alikuwa na ushawishi mkubwa kwa vijana, hasa kusini mwa mji wa Djibo mkoani Soum.
Kwa mujibu wa duru za jeshi, gaidi huyo alihusika katika mashambulizi kadhaa yaliyofanywa katika ukanda wa Sahel, hasa kwenye barabara ya Bourzanga-Djibo.../