Al Azhar yalaani kuvunjiwa heshima Mtume Muhammad SAW nchini India
Chuo Kikuu cha Kiislamu ya al Azhar cha nchini Misri kimelaani utovu wa adabu wa wanachama wawili wa chama tawala cha BJP cha kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri kimetoa taarifa nzito na yenye maneno makali ya kulaani utovu wa adabu uliofanywa na wanachama hao waandamizi wa chama tawala cha BJP cha India na kusisitiza kuwa, vitendo kama hivyo ni mfano wa wazi wa ugaidi ambao lengo lake ni kuitumbukiza dunia nzima katika vita angamizi.
Taarifa hiyo imeitaka jamii ya kimataifa kusimama imara kukabiliana na hatari zinazosababishwa na maadui hao wa Uislamu na ubinadamu.
Katika mdahalo wa televisheni, msemaji wa chama tawala cha India, BJP, Nupur Sharma alitoa matamshi ya kichochezi dhidi ya Mtume wa Uislamu, ambayo yamelaaniwa kote India na kuzusha ghasia nchini humo.
Juzi Jumapili chama cha BJP kilitangaza kusimamisha uanachama wa Sharma na kujiweka mbali na matamshi yake ya chuki.
Balozi wa India nchini Misri naye ameelezea kusikitishwa na kitendo hicho cha wanachama wa chama tawala cha BJP huko India na kusema kuwa ni jambo lisilokubali kabisa kumvunjia heshima Mtume wa Uislamu.
Amesema, msimamo wa serikali ya India ni kuheshimu dini zote na kwamba mtumishi yeyote wa serikali haruhusiwi kumvunjia heshima mtu yeyote. Amesema, waliomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW huko India ni wanachama wa wa chama cha BJP, si watumishi serikalini.
Chama cha BJP kimemfukuza kazi pia Naveen Kumar Jindal ambaye anasimamia kitengo cha habari cha chama hicho mjini New Delhi na ambaye pia alituma ujumbe uliomvunjia heshima Mtume Muhammad SAW katika ukurasa wake wa Twitter na baadaye akalazimika kuufuatia kutokana na kuongezeka malalamiko dhidi yake.