Kuanza mazungumzo baina ya Sudan na Sudan Kusini
Mazungumzo kati ya maafisa wa Sudan na Sudan Kusini yalianza tena jana Jumatatu ya tarehe 6 Juni katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Tangu ilipoundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Sudan Kusini, hii ni mara ya kwanza kwa mawaziri wa Mambo ya Nje, Ulinzi, Mambo ya Ndani na wa Mafuta wa Sudan Kusini kufanya safari nchini Sudan ili kufanya mazungumzo juu ya namna kutatua hitilafu zilizopo baina ya nchi mbili.
Uainishaji mipaka na mgawanyo wa mapato ya mauzo ya mafuta ya eneo la kusini ni miongoni mwa ajenda kuu za mazungumzo baina ya maafisa wa nchi hizo mbili yanayofanyika huko Khartoum.
Lengo la mazungumzo ya sasa limeelezwa kuwa ni kumaliza hitilafu za masuala ambayo yamebaki bila ya kupatiwa utatuzi hadi sasa tangu Sudan Kusini ijitangazie uhuru. Sudan Kusini ilijitenga na Sudan tarehe 9 Julai mwaka 2011 na kutangazwa kuwa taifa huru.
Katika mazungumzo ya pamoja waliyofanya na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ibrahim Ghandour na mwenzake wa Sudan Kusini Deng Alor wamesisitiza kuwa nchi zao zingali zinahitilafiana katika mambo kadhaa.
Alor ameeleza kuwa katika safari yake hiyo mjini Khartoum amebeba ujumbe wa Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kwa Rais Omar al-Bashir wa Sudan ambao unasisitiza juu ya kutatuliwa haraka hitilafu zilizopo kati ya nchi mbili.
Sudan na Sudan Kusini zinahitilafiana katika masuala kadhaa, muhimu zaidi likiwa ni la umiliki wa eneo la mpakani lenye utajiri wa mafuta la Abyei, ambalo hivi sasa linadhibitiwa na vikosi vya usalama vya serikali ya Khartoum.
Kwa mujibu wa vipengele vya hati ya makubaliano iliyosainiwa na nchi mbili Oktoba 14 mwaka 2015, serikali ya Sudan Kusini itapaswa kulipa gharama ya kutumia mabomba ya kusafirishia mafuta kwa ajili ya kupitishia mafuta yake nchini Sudan. Mabomba hayo ya mafuta yanapitia Sudan; na Sudan Kusini inayahitajia kwa ajili ya kusafirishia mafuta yake.
Katika safari yao nchini Sudan, maafisa wa kamisheni ya usalama na ya kisiasa ya Sudan Kusini wanakusudia kutoa msukumo zaidi kwa ajili ya kuharakisha utekelezaji wa vipengee vya hati hiyo ya makubaliano iliyosainiwa mwaka jana.
Katika mazungumzo hayo yaliyopita Sudan na Sudan Kusini zilizungumzia uainishaji mpaka wa asilimia 80 ya eneo la mpaka wa pamoja wa nchi mbili.
Katika mazungumzo yanayoendelea hivi sasa mjini Khartoum, mawaziri wa Ulinzi, Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani na Mafuta wa nchi mbili wanapaswa kujadiliana juu ya namna ya kumaliza hitilafu zilizosalia.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ibrahim Ghandour amesisitiza kuwa kipaumbele cha kwanza kwa serikali ya nchi hiyo ni kurejesha katika hali ya kawaida uhusiano wake na Sudan Kusini ambayo ina mafungamano ya kihistoria na Sudan.../