DRC yakosoa ripoti ya HRW kwamba askari wake waliua CAR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8902-drc_yakosoa_ripoti_ya_hrw_kwamba_askari_wake_waliua_car
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekosoa ripoti ya hivi karibuni ya Human Rights Watch iliyodai kuwa askari wa nchi hiyo wa kulinda amani huko Jamhuri ya Afrika ya Kati waliua na kukandamiza raia wasio na hatia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 10, 2016 09:46 UTC
  • DRC yakosoa ripoti ya HRW kwamba askari wake waliua CAR

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekosoa ripoti ya hivi karibuni ya Human Rights Watch iliyodai kuwa askari wa nchi hiyo wa kulinda amani huko Jamhuri ya Afrika ya Kati waliua na kukandamiza raia wasio na hatia.

Thierry Moungalla, Waziri wa Mawasiliano wa Kongo DR amesema ripoti hiyo ya Human Rights Watch haina ukweli wowote na imeegemea upande mmoja. Hata hivyo Pierre Mabiala, Waziri wa Sheria wa nchi hiyo amesema serikali itabuni kamisheni maalumu katika mahakama ya jinai kuchunguza madai hayo lakini amesisitiza kuwa, kwa sasa wanaihesabu ripoti hiyo kama madai tu ambayo hayana msingi wala ithibati.

Jumanne iliyopita, Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch liliwatuhumu askari wa kulinda amani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaohudumu katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi za Afrika AU kuwa wamehusika na mauaji ya raia 18 wa nchi hiyo wakiwemo wanawake na watoto. Tuhuma hizo zimetolewa dhidi ya askari hao wa Kongo DR katika hali ambayo hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti iliyoashiria kesi 44 za ufisadi wa kimaadili wa askari wake wanaohudumu katika pembe tofauti za dunia na hasa katika katika kikosi cha MINUSCA katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Jinai nyingi za ubakaji na mauji dhidi ya wanawake na watoto wadogo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati zimekuwa zikihusishwa na askari wa kulinda amani wa Ufaransa na DRC.