Msemaji wa Rais wa Afrika Kusini: Ramaphosa hatajiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i91290-msemaji_wa_rais_wa_afrika_kusini_ramaphosa_hatajiuzulu
Msemaji wa Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye yupo chini ya mashinikizo ya kutakiwa ajiuzulu kutokana na kashfa ya ufisadi inayomzunguka amesisitiza kuwa kiongozi huyo hatoachia ngazi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 04, 2022 03:32 UTC
  • Msemaji wa Rais wa Afrika Kusini: Ramaphosa hatajiuzulu

Msemaji wa Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye yupo chini ya mashinikizo ya kutakiwa ajiuzulu kutokana na kashfa ya ufisadi inayomzunguka amesisitiza kuwa kiongozi huyo hatoachia ngazi.

Vincent Magwenya, Msemaji wa Rais wa Afrika Kusini aliwaambia waandishi wa habari kupitia arafa jana Jumamosi kuwa, Ramaphosa hatajiuzulu kwa kutegemea ripoti iliyojaa dosari.

Amesema Rais wa Afrika Kusini ataka rufaa dhidi ya ripoti hiyo yenye makosa ya wazi dhidi yake, kwa maslahi ya muda mrefu na kwa lengo la kulinda demokrasia endelevu ya kikatiba nchini humo.

Ramaphosa anakabiliwa na miito mbalimbali inayomtaka ajiuzulu baada ya uchunguzi wa Bunge kubaini kuwa huweda alikiuka sheria za kupambana na ufisadi kuhusiana na wizi wa mamilioni ya dola katika shamba lake la Phala Phala.

Kamati ya uchunguzi ya Bunge la Afrika Kusini iliibua maswali katika ripoti yake kuhusu chanzo cha fedha hizo za Cyril Ramaphosa na kwa nini kiasi chote hicho hakikutangazwa kwa mamlaka husika za fedha.

Maandamano dhidi ya rais wa Afrika Kusini

Rais wa Afrika Kusini kwa upande wake amekanusha tuhuma za ufisadi dhidi yake na kusema alizipata kutokana na mauzo ya wanyama wa shambani kwake. Wakati huo huo, vyama vya upinzani na wapinzani wa Ramaphosa ndani ya chama tawala cha ANC vimetoa wito wa kujiuzulu Ramaphosa. 

Wanachama wa ANC wanatazamiwa kukutana leo katika mkutano wa Kamati Maalumu ya Kitaifa ya Kazi kujadili kadhia ya Ramaphosa. Baada ya kikao cha leo, Kamati Kuu ya Taifa ya chama hicho kinatazamiwa kukutana hapo kesho kuamua juu ya hatua itakayomchukuliwa Rais huyo wa Afrika Kusini.