Wananchi wa Tunisia waandamana tena dhidi ya Rais Kais Saied
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i92902-wananchi_wa_tunisia_waandamana_tena_dhidi_ya_rais_kais_saied
Kwa mara nyingine tena wananchi wa Tunisia wamefanya maandamano makubwa wakimtaka Rais Kais Saied wa nchi hiyo na serikali yake wajiuzulu, kwa kushindwa kuinasua nchi hiyo kutoka kwenye mgogoro wa kisiasa na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 15, 2023 06:55 UTC
  • Wananchi wa Tunisia waandamana tena dhidi ya Rais Kais Saied

Kwa mara nyingine tena wananchi wa Tunisia wamefanya maandamano makubwa wakimtaka Rais Kais Saied wa nchi hiyo na serikali yake wajiuzulu, kwa kushindwa kuinasua nchi hiyo kutoka kwenye mgogoro wa kisiasa na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii.

Maandamano hayo yalifanyika jana jijini Tunis na katika miji mingine ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, sambamba na maadhimisho ya mwaka wa 12 tangu kuangushwa kwa utawala wa kidikteta wa Zine El Abidine Ben Ali, kupitia mapinduzi ya umma ya mwaka 2011.

Maelfu ya waandamanaji hao waliokuwa na ghadhabu walikabiliana na maafisa wa polisi katika barabara ya Habib Bourguiba katikati mwa Tunis, nje ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mwanamke mmoja aliyeshiriki maandamano hayo kwa jina la Nouha amewaambia waandishi wa habari kuwa, "Mapinduzi (ya Kais Saied) hayajatuletea kitu kingine ghairi ya njaa na ukata, napaswa kulisha familia ya watu 13."

Maandamano yamekuwa yakifanyika mara kwa mara nchini Tunisia kupinga hatua  ya Rais Kais Saied kutwaa madaraka kamili ya nchi mnamo Julai mwaka 2021.

Waandamanaji pia wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa  chakula, mafuta na uingiliaji wa madola ya kigeni hasa Ufaransa katika mambo ya ndani ya nchi hiyo. Harakati ya Demokrasia ya Tunisia imewataka wananchi wa nchi hiyo kuendeleza mashinikizo dhidi ya serikali ya Rais Kais Saied ili kuhakikisha kunafanyika mageuzi.

Maandamano haya yanafanyika katika hali ambayo, muungano mkubwa wa Wafanyakazi Tunisia (UGTT) umetangaza mkakati wake wa kuendesha mgomo wa siku mbili tarehe 25 na 26 mwezi huu wa Januari ili kuendelea kuishinikiza serikali ya Kais Saied.