Kenya na Somalia zakubaliana kushirikiana zaidi ili kuboresha hali ya usalama
Serikali ya Kenya imetangaza kufungua tena mpaka wa nchi kavu wa nchi hiyo na Somalia kwa lengo la kuboresha hali ya usalama katika mipaka hiyo.
Mwaka wa 2012, Kenya ilifunga vivuko vyake vyote vya mpakani kati yake na Somalia ili kuzuia kupenya magaidi wa al Shabaab katika ardhi yake.
Makundi yenye silaha ambayo yanajihusisha na biashara ya silaha, chakula na binadamu yamemekuwa yakihatarisha usalama wa maeneo ya mpakani mwa Kenya na Somalia kwa miaka mingi. Ukosefu huo wa usalama unahusika moja kwa moja na mashambulio ya kigaidi ya genge la al Shabab ambalo limepanua wigo wa mashambulizi yake kutoka Somalia hadi ndani ya ardhi ya Kenya.
Shirika la habari la Tasnim liliripoti habari hiyo jana Jumatatu na kuinukuu serikali ya Kenya ikitangaza kwamba, baada ya kupita miaka 10 sasa kivuko cha mpakani cha Mandera kimefunguliwa tena.
Katika taarifa yake hiyo, serikali ya Kenya imesisitiza kuwa, lengo la kufunguliwa kivuko hiyo ni kupambana na ongezeko la magendo ya binadamu na chakula. Kivuko cha Mandera kimefunguliwa tena baada ya mashauriano kati ya maafisa wa ngazi za juu wa Kenya na Somalia.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imeashiria pia harakati za genge la ala Shabaab katika mikoa ya kaskazini-mashariki mwa Kenya ambayo wakazi wake wengi ni jamii ya Kisomalia na kusisitiza kuwa, itatumia vikosi vya kujitolea vya wananchi kupambana na al Shabaab. Mbinu hiyo inaonekana kufanya vizuri nchini Somalia ambapo serikali ya nchi hiyo imeripotiwa kupata ushindi mkubwa dhidi ya magaidi hao.