Jun 19, 2016 07:55 UTC
  • Mashirika ya kijamii Nigeria: Boko Haram ni hatari kwa watoto wadogo

Shirika moja lisilo la kiserikali nchini Nigeria kwa kifupi PIN, limeonya juu ya mwenendo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram wa kuwatumia watoto wadogo katika jinai zake.

Hayo yamesemwa na Hussein Abdou, kiongozi mwandamizi wa shirika hilo nchini Nigeria na kuongeza kuwa, katika kipindi cha miaka sita iliyopita, karibu watoto milioni 15 wa nchi hiyo waliathiriwa kwa namna tofauti na hujuma za kundi hilo. Abdou amesisitiza kuwa, watoto milioni saba kati yao wanaishi katika hali ngumu huku wengine elfu 20 wakiwa tayari wamepoteza maisha yao katika machafuko yanayotokana na wanachama wa genge hilo. Aidha afisa huyo wa shirika la PIN ameongeza kuwa, aghlabu ya watoto ambao bado wanashikiliwa na wanachama wa Boko Haram wanakabiliwa na matatizo ya chakula, kuzuiwa kuendelea na masomo na pia kutumiwa vibaya kijinsia. Kabla ya hapo serikali ya Nigeria ilitangaza kuwa, jumla ya shule 300 katika jimbo la Borno zimeharibiwa kikamilifu na mashambulizi ya magaidi hao. Kadhalika walimu 196 na watoto 314 wameuawa katika hujuma hizo.

Tags