Apr 18, 2023 07:05 UTC
  • Zaidi ya watu 180 wameuawa katika mapigano Sudan

Takriban watu 185 wameuawa na wengine 1,800 kujeruhiwa katika mapigano ambaye yanaendelea kwa muda wa siku nne sasa kati ya pande zinazohasimiana nchini Sudan. Hayo ni kwa mujibu wa mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan huku jamii ya kimataifa ikitoa wito kwa pande hasimu kusitisha mapigano.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini  Sudan, Volker Perthes amesema kwamba hali ni tete sana Sudan, na ni vigumu sana kusema hivi sasa uhasama umechukua mkondo gani, huku mapigano ya yakiendelea baina ya askari wa jeshi la taifa na askari wa Vikosi vya Msaada wa Dharura (RSF).

Pande hizo mbili hasimu zinatumia vifaru, mizinga na silaha nyingine nzito katika maeneo yenye watu wengi. Ndege za kivita pia zimetumika huku upande wa pili nao ukitumia marokeo ya kutungua ndege.

Kuzuka kwa ghasia za ghafla mwishoni mwa juma kati ya majenerali wawili wakuu wa taifa hilo, kila mmoja akiungwa mkono na makumi ya maelfu ya askari waliokuwa na silaha nzito, kulipelekea mamilioni ya watu washindwe kutoka majumbani mwao huku kukiwa na uhaba wa bidhaa muhimu za matumizi katika maeneo mengi.

Mapigano ya kuwania madaraka ni baina Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kamanda wa vikosi vya jeshi ambaye pia ni mtawala wa Sudan, na  Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, mkuu Vikosi vya Msaada wa Dharura (RSF). Majenerali hao wawili ni washirika wa zamani kwani walishirikiana kutekeleza  mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 2021.

Ghasia hizo zimeibua wasiwasi wa vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati Wasudan walipokuwa wakijaribu kufufua serikali ya kidemokrasia ya utawala wa kiraia baada ya miongo kadhaa ya utawala wa kijeshi.

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan

Siku ya Jumatatu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alitoa wito tena kwa pande zinazozozana "kusimamisha uhasama mara moja" akionya kwamba kuongezeka mapigano kutaivuruga nchi hiyo na eneo hilo la Afrika."

Taasisi za kikanda zikiwemo Umoja wa Afrika, kundi la kikanda la IGAD, na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League), zimesema zinazungumza na mahasimu mbalimbali hasa majenerali hao wawili, kujaribu kusitisha mapigano.

Wakati huo huo, jeshi la Sudan limeitangaza RSF kuwa kundi la waasi na kuamuru kuvunjwa kwake siku ya Jumatatu.

Muungano wa madaktari nchini Sudan umeonya kwamba mapigano hayo "yameharibu pakubwa" hospitali nyingi mjini Khartoum na miji mingine, huku zingine zikiwa haziwezi kutoa huduma.

Shirika la Afya Duniani lilikuwa tayari limeonya kwamba hospitali kadhaa kati ya tisa za Khartoum zinazopokea raia waliojeruhiwa "zimeishiwa damu, vifaa vya kutia mishipani, na vifaa vingine muhimu".

Tags