Raila Odinga kuanza tena maandamano dhidi ya serikali ya Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i96618-raila_odinga_kuanza_tena_maandamano_dhidi_ya_serikali_ya_kenya
Mrengo wa upinzani nchini Kenya umesema kuwa umepanga kuanza tena maandamano dhidi ya serikali kuanzia tarehe Pili mwezi ujao wa Mei; ikiwa zimepita karibu wiki tatu tangu usimamishe maandamano yake dhidi ya serikali ya Rais William Ruto ili kutoa fursa ya kushiriki kwenye mazungumzo na serikali.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 24, 2023 12:35 UTC
  • Raila Odinga
    Raila Odinga

Mrengo wa upinzani nchini Kenya umesema kuwa umepanga kuanza tena maandamano dhidi ya serikali kuanzia tarehe Pili mwezi ujao wa Mei; ikiwa zimepita karibu wiki tatu tangu usimamishe maandamano yake dhidi ya serikali ya Rais William Ruto ili kutoa fursa ya kushiriki kwenye mazungumzo na serikali.

Dennis Onyango, msemaji wa Raila Odinga kiongozi mkongwe wa upinzani Kenya ambaye aliratibu maandamano kadhaa ya kupinga ughali wa maisha huko Kenya mwezi Machi mwaka huu ameeleza kuwa, wanapanga kuanza tena maandamano yao kuanzia Mei 2. 

Hata hivyo msemaji huyo wa Raila Odinga hakusema ni kwa nini wameamua kuanza tena maandamano. Itakumbukwa kuwa Odinga alikuwa akiitisha maandamano mara mbili kwa wiki nchini Kenya yaani katika siku za Jumatatu na Alhamisi tangu Machi 20 akimtuhumu Rais wa nchi hiyo, William Ruto, kuwa aliiba kura katika uchaguzi wa rais wa Agosti mwaka jana.

Vilevile anamkosoa Rais wa Kenya kwamba ameshindwa kuzuia kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali nchini humo.

Polisi ya Kenya imepiga marufuku maandamano ya upinzani.

Raila Odinga (78) ambaye amegombea kiti cha urais kwa mara kadhaa na kushindwa na wapinzani wake, alichukua uamuzi wa kusitisha maandamano ili kushiriki katika mazungumzo na serikali. 

Kwa upande wake, Rais William Ruto amewatolea wito wananchi kuheshimu utawala wa sheria huku Kamati ya Bunge ya pande mbili ikichunguza uwezekano wa kurekebisha kanuni za uchaguzi.

Watu watatu akiwemo afisa wa polisi walipoteza maisha katika maandamano ya upinzani hivi karibuni ambapo pia vitendo vya wizi na uporaji viliripotiwa. Ripoti za awali zilisema kuwa, waandamanaji waliuawa katika ufyatuaji risasi wa polisi katika mji wa Kisumu huko magharibi mwa Kenya ambayo ni ngome kuu ya upinzani.

Maandaano ya karibuni mjini Kisumu