May 14, 2023 13:58 UTC
  • Kupuuza Misri takwa la Marekani dhidi ya Russia; ishara ya kufifia ushawishi wa Marekani

Gazeti la Wall Street Journal limetangaza kuwa, Misri imepuuzilia mbali takwa la Marekani kwa nchi hiyo la kutoruhusu ndege za kijeshi za Russia kupita katika anga yake.

Misri inahesabiwa kuwa mmoja wa waitifaki wakongwe wa Marekani ambaye kwa mwaka hupokea zaidi ya dola bilioni moja kutoka kwa Washington kama msaada katika uga wa masuala ya kijeshi. Pamoja na hayo, katika kipindi cha utawala wa Rais Abdul-Fattah al-Sisi, Misri imeonekana kugeuza mwelekeo na kuimarisha zaidi uhusiano wake na Russia hasa katika miaka michache ya hivi karibuni.

Gazeti hilo limewanukuu viongozi wa Misri na Marekani ambao majina yao hayakutajwa na kuandika: Misri haijatoa jibu chanya kwa takwa la Marekani kufunga anga yake na kutoruhusu ndege za kijeshi za Russia kupita hapo. Takwa hilo lililokataliwa na Misri lilikuwa likilenga kudhoofisha harakati za kijeshi za Russia kabla ya mashambulio ya majibazano yaliyokuwa yakitarajiwa na Ukraine. Ndege za kijeshi baina ya Russia na Syria ziliruka bila ya kizuizi.  Anga ya Misri inahesabiwa kuwa moja ya korido muhimu na zenye uhai baina ya Russia na nchi hiyo huko Syria.

 Kituo cha kijeshi la Hmeimim kilichoko katika pwani ya Bahari ya Mediterania huko nchini Syria ni moja ya tasisi muhimu za kijeshi za Russia nchini Syria. Ndege za kijeshi la Russia baada ya mwaka jana kufungiwa anga na baadhi ya mataifa, zililazimika kukata masafa ya maili 2000 ili kufika katika kituo chao cha kimkakati nchini Syria. Kama Misri ingefuata takwa la Marekani, basi ndege za Russia zingelazimika kukata masafa marefu zaidi ili ziingie Afrika. Viongozi wa Marekani walidai kwamba, Russia inahamisha silaha zake katika kambi yake huko Syria na kuzipeleka katika medani ya vita huko Ukraine. Hata hivyo, hadi sasa madai hayo hayajathibitishwa na Russia imeyakadhibisha vikali.

Inaonekana kuwa, kutopewa jibu chanya Marekani na Misri kuhusiana na takwa lake kwa Cairo la kutoruhusu ndege za kijeshi za Russia kupita katika anga yake, ni ishara nyingine ya kupungua ushawishi wa Washington miongoni mwa waitifaki wake katika eneo la Asia Magharibi na kaskazini mwa Afrika. Nukta muhimu ni hi kwamba, hatua ya Misri ya kutoa kibali kwa ndege za Russia cha kupita katika anga yake na kuelekea Syria, sio uamuzi wa kwanza au wa pili wa Cairo wa kuwa pamoja na Moscow.

Kabla ya hapo pia, katika nyaraka za siri za Pentagon zilizofichuliwa hivi karibuni ilifahamika kuwa, Rais Abdul-Fattah al-Sisi alikuwa na mpango wa kuipatia Russia makumi ya maelfu ya maroketi wakati wa kuendelea vita vya Ukraine. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, al-Sisi aliwapa maagizo maafisa husika katika serikali yake wafanye kuwa jambo la siri suala la uzalishashaji mkubwa wa maroketi ili kuepuka kukabiliwa na matatizo kutoka kwa madola ya Magharibi.

Inaonekana kuwa, mataifa ya Kiarabu ambayo ni waitifaki na washirika wa Marekani ikiwemo Saudi Arabia pamoja na washirika wake wa eneo la kusini mwa Ghuba ya Uajemi na vilevile Misri katika miaka ya hivi karibuni yamefuatilia mwenendo wa kujitenga na misimamo ambayo iko kinyume na matakwa na malengo ya Marekani.

Kubadilisha mtazamo washirika wa kieneo wa Marekani kama Saudi Arabia na nchi nyingine wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na kufanya juhudi za kupunguza mizozo na mivutano ya kieneo sambamba na kurejesha uhusiano wa kawaida na Iran ni mambo ambayo yana uhusiano wa moja kwa moja na suala la mataifa hayo kutokuwa na imani tena na Washington.

John F. Kennedy Junior anasema: Kuporomoka ushawishi wa Marekani kwa Saudi Arabia na hatua ya utawala huo wa Kifalme ya kuunda muungano mpya na China na Iran, ni ishara ya wazi kabisa ya kushindwa kwa fedheha mikakati ya Marekani ya kulinda mamlaka ya kuwa na sauti ulimwenguni kwa kutumia njia za kijeshi. Kuondoka kwa madhila na vichwa chini askari wa Marekani huko nchini Afghanistan ambapo kwa mujibu wa Rais Joe Biden hilo lilifanyika kwa leo la kuinasua Washington na vita visivyo na kikomo, kwa mtazamo wa walimwengu  hata waitifaki wa Washington hiyo ni ishara ya kupoteza nafasi iliyokuwa nayo Marekani ya kuwa nguvu yenye taathira ulimwenguni.

Tags