Watu wasiojulikana washambulia kituo cha mafuta cha Shell Nigeria
Polisi nchini Nigeria imethibitisha kujiri shambulizi dhidi ya kituo cha mafuta kinachomilikiwa na shirika la mafuta la Shell katika jimbo la Imo, kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Andrew Enwerem, msemaji wa jeshi la polisi katika mji wa Owerri, katikati mwa jimbo hilo la Imo, amenukuliwa akisema kuwa, polisi imepata taarifa ya hujuma hiyo dhidi ya kituo hicho cha mafuta. Amesema shambulio hilo lililotekelezwa jana, lilikuwa kubwa kiasi cha kusababisha uharibifu mkubwa na kwamba hadi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika. Licha ya kwamba kundi la ulipizaji kisasi la Niger Delta limehusika katika hujuma kadhaa dhidi ya taasisi za mafuta na gesi nchini humo, lakini safari hii halijatangaza kuhusika na hujuma hiyo. Hivi karibuni wanachama wa kundi hilo la Niger Delta walikataa pendekezo la serikali kuu ya Abuja la kufanya mazungumzo yenye lengo la kumaliza machafuko yanayoendelea kusini mwa nchi.