Sababu za kusalia imara Muqawama-2
(last modified Sun, 17 Nov 2024 02:39:09 GMT )
Nov 17, 2024 02:39 UTC
  • Sababu za kusalia imara Muqawama-2

Hamjambo na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi chetu cha leo ambacho kinaendelea kuzungumzia sababu za kuendelea kusimama imara kambi ya Muqawama dhidi ya mabeberu na utawala wa Kizayuni wa Israel...

Watu, misimamo na maoni ya umma huwa na nafasi muhimu katika tukio lolote. Kwa mfano tu, uungaji mkono wa watu kwa vikosi vya jeshi ni moja ya sababu kuu za ushindi wa jeshi lolote katika vita. Kwa sababu hiyo, hata majeshi ambayo hayana nafasi wala ushawishi baina ya watu, hutumia propaganda na fedha nyingi kuhalalisha utendaji wake na kujidhihirisha kama mtetezi wa maslahi ya taifa ili kupata uungaji mkono wa umma. Kwa mfano, pamoja na kwamba watu wa Marekani hawafurahishwi na ukweli kwamba sehemu kubwa ya kodi zao zinatumika katika masuala ya kijeshi na hatua za kujitanua, lakini vyombo vingi vya habari vya nchi hiyo vinaeneza propaganda kuwa jeshi la nchi hiyo linapigana nje ya nchi ili kudhamini usalama wa kitaifa wa Marekani na kutetea demokrasia na haki za binadamu! Lakini kwa harakati za ukombozi na uhuru, ni muhimu sana kuwa na uungaji mkono wa watu ili kuendelea kuwepo na kuzidisha ari na nguvu ya wapiganaji. Kwa sababu, wanapigania uhuru wa taifa na nchi yao kutoka kwenye makucha ya wakoloni na mabeberu. Vivyo hivyo makundi ya Muqawama, ambayo wapiganaji wake wanatokana na makundi ya wananchi wa kawaida, wanapigana kwa ajili ya kuwakomboa watu kutoka kwenye minyororo ya wavamizi na mabeberu.

Wanachama wa makundi ya Muqawama ni watu wenye imani na maono ya mbali ambao kwa kawaida wanajali zaidi suala la kuokoa nchi na watu wao na kupigana na dhalimu na wavamizi. Wengi wao waliuawa shahidi katika njia hiyo, na wengine wako tayari kusabilia maisha yao kwa ajili ya malengo yao matakatifu. Ni kawaida kwamba, watu wanaunga mkono kikamilifu vikosi hivyo vya kujitolea na kupigana Jihadi. Tunapotazama rekodi za wanamuqawama hawa katika nchi tofauti tunaona jinsi walivyotetea watu wao na nchi zao bila kutarajia lolote kutoka kwa watu. Kwa muda wa miaka minane, wapiganaji wa Iran walilishinda jeshi la Saddam lililokuwa limejizatiti kwa silaha za kisasa, ambalo lilikuwa likisaidiwa kikamilifu na nchi za Magharibi, wakiwa na rasilimali ndogo na kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu na uungaji mkono wa watu. Baada ya vita, vikosi vya jeshi la Iran vilizidisha nguvu zao kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya adui, kulinda watu wa Iran na kutetea wanaodhulumiwa kote duniani. Katika baadhi ya matukio, majeshi ya Iran yalikwenda Iraq na Syria kwa ombi la serikali za nchi hizo na kuzisaidia kukabiliana na makundi ya waasi, ya kigaidi na kitakfiri.

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na Jihad Islami ya Palestina pia ni makundi ya watu yaliyoundwa kwa ajili ya kupambana na dhulma, uvamizi na ukatili wa utawala ghasibu wa Israel. Vikosi vya Muqawama wa Kiislamu vya Palestina vinaundwa na vijana jasiri na wazoefu ambao wameamua kuhatarisha maisha yao kukabiliana na askari wa Kizayuni wenye silaha za kisasa na wamekuwa wakipambana nao kwa miaka mingi, kiasi kwamba sasa utawala wa kibaguzi wa Israel unakiri kwamba licha ya kuwa silaha na zana zote hizo na himaya na misaada ya isiyo na kikomo ya Marekani umeshindwa kuangamiza makundi hayo ya Muqawama na mapambano. Hapana shaka yoyote kwamba, iwapo wananchi wa Palestina hususan wa Gaza wasingewaunga mkono Mujahidina wa Hamas, harakati hiyo ingekumbwa na matatizo makubwa na operesheni zake zingefeli. Lakini Wapalestina wanajua kuwa, bila ya mapambano ya vikosi vya Muqawama, hali yao ingekuwa mbaya zaidi kuliko ilivyo sasa.

Wanamapambano wa Hamas ya Palestina 

Lebanon pia imeonja uchungu wa kukaliwa kwa mabavu na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel. Lakini katika nchi hii pia, vijana wa matabaka mbalimbali ya wananchi walibeba bendera ya kupigana dhidi ya askari wa utawala huo vamizi kwa kuanzisha harakati ya "Hizbullah", na baada ya miaka 8, mwaka 2000, walililazimisha jeshi la Israel kuondoka Lebanon kwa madhila. Kwa mara nyingine tena, vijana wa Hizbullah wamelishinda jeshi hilo vamizi na hivi sasa wako katika vita vya kijasiri na visivyo na usawa na utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kuwatetea watu madhulumu wa Gaza.

Mujahidina wa Iraq pia baada ya kukaliwa kwa mabavu nchi yao na Marekani mwaka 2003, hatua kwa hatua waliunda makundi yaliyotaka kufukuzwa  wanajeshi hao vamizi wa Kimarekani katika nchi yao. Ingawa serikali ya Marekani ililazimika kuondoa sehemu kubwa ya vikosi vyake vya jeshi huko Iraq chini ya mashinikizo ya Mhimili wa Muqawama, lakini bado ina askari kadhaa huko Iraq, na kwa sababu hiyo, wanaendelea kushambuliwa na wanamapambano wa Iraq. Wakati huo huo vikosi vya Muqawamavya Iraq havijawasahau ndugu zao wa Palestina, na vinashambulia vituo nyeti vya utawala wa Kizayuni kwa makombora na ndege zisizo na rubani.

Yemen ni nchi nyingine ya Kiislamu ambayo imekuwa katika vita visivyo na mlingano dhidi ya muungano wa Kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia tangu 2012. Hata hivyo, Mujahidina wa Yemen hawakusalimu amri, bali walipata ushindi muhimu na kuwalazimisha maadui wa ndani na wa nje kurudi nyuma. Wapiganaji shupavu wa Yemen pia wameonyesha uungaji mkono wao wa kivitendo na madhubuti kwa Palestina na watu madhulumu wa Gaza, na wamekuwa wakishambulia bila ya woga meli zinazoelekea katika bandari za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wanamuqawama wa Yemen 

Kwa miongo kadhaa serikali ya Marekani na utawala wa Kizayuni zimekuwa adui wa pamoja wa watu wa eneo la Magharibi mwa Asia; na utawala huo umekuwa ukifanya jinai zisizo na kifani katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa miaka mingi kwa msaada kamili wa Marekani. Kwa kuzingatia Aya nyingi za Qur'ani na Hadithi za Mtume (saw), wapiganaji wa Islamic Resistance Front pia wanapambana dhidi mashetani hao wawili katika nyanja mbalimbali. Miongozi mwa Aya hizo ni ile inayosema: Na mna nini hampigani katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanaoonewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola wetu Mlezi! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anayetoka kwako, na tujalie tuwe na wa kutunusuru anayetoka kwako.

Kwa kuzingatia masuala haya, ni wazi kuwa mtaji mkubwa wa Muqawama ni uungaji mkono mkubwa na wa pande zote wa wananchi.