Sep 28, 2023 15:24 UTC
  • Ghalibaf: Nchi za Afrika kwa Iran ni muhimu sana kama ilivyo kundi la BRICS

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema katika mazungumzo na wanaharakati na wabunge wa Afrika Kusini kwamba, Tehran inaamini kuwa, umuhimu wa nchi za Afrika hususan Afrika Kusini ni mkuubwa na ni sawa na umuhimu wa kundi la BRICS, kwa Iran. 

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Mohammad Baqir Qalibaf, ambaye amekwenda nchini Afrika Kusini kushiriki Mkutano wa 9 wa Bunge la BRICS amesema hayo na kuongeza kuwa, ushirikiano kati ya Iran na Afrika Kusini hususan katika kurahisisha mawasiliano kati ya wanaharakati wa kiuchumi wa nchi hizo mbili, kuzisaidia nchi za Afrika kuendeleza biashara huria, kusaidia wanyonge hasa wa Palestina, kupigania kuweko mfumo wa haki wa utawala duniani na kutumia fursa ya uwanachama wa BRICS ni katika masuala muhimu kwa pande zote mbili ambayo yanaweza kuzidisha ushirikiano wa Iran na Afrika Kusini na nchi nyingine za Afrika.

Katika mazungumzoa hayo, Spika wa Bunge la Iran aidha amesema: Mataifa mawili ya Iran na Afrika Kusini yana utamaduni na ustaarabu mkongwe hasa katika kupambana na dhulma na madhalimu na ubaguzi wa rangi. Ni kwa sababu hiyo ndio maana katika ile miezi ya awali kabisa ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Imam Khomeini (MA) alitoa amri ya kimapinduzi ya kukata uhusiano na tawala mbili za kibaguzi na kidhalimu yaani utawala wa makaburu wa Afrika Kusini na utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Kwa hakika, uamuzi huo wa Imam Khomeini ulitokana na imani thabiti ya kidini na hisia za kibinadamu alizokuwa nazo na mtazamo huo unaendelea hivi leo kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Spika Ghalibar  amegusia pia malengo ya pamoja ya mataifa ya Iran na nchi za Afrika pamoja na Ulimwengu wa Kiislamu na kusema: Lazima nisisitizie nukta hii muhimu kwamba kupata ushindi katika jambo fulani ni rahisi zaidi kuliko kuendelea na kuuhifadhi ushindi huo. Sababu yake ni kuwa, baada ya ushindi huo, majukumu yanaongezeka na kwa hivi sasa ni lazima tuendeleze mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na dhulma inayoendelea kufanywa na madhalimu udhidi ya wanadamu wengine. 

Tags