Sep 30, 2023 07:31 UTC
  • Iran yatangaza utayari wa kuimarisha uhusiano wake na Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesema, Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuimarisha uhusiano na maelewano ya pande mbili kati yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania January Yusuf Makamba, ambapo sambamba na kumpongeza January kwa kuteuliwa kuwa waziri mpya wa mambo ya nje wa nchi hiyo, ameashiria historia ya uhusiano wa nchi mbili pamoja na kuwepo kwa fursa mbalimbali, na kusisitizia utayari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuimarisha uhusiano na maelewano baina yake na Tanzania hususan ushirikiano wa kiuchumi, sayansi na teknolojia.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa kheri na baraka pia kwa serikali na Waislamu wa Tanzania kwa mnasaba wa maadhimisho ya Maulidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

Kwa upande wake, waziri mpya wa mambo ya nje wa Tanzania ametoa shukurani kwa waziri mwenzake wa Iran na kueleza utayari wa kustawisha uhusiano kati ya nchi mbili.

Vilevile January ametilia mkazo mwaliko uliotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwa Seyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kutembelea Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao hayo, mawaziri hao wa mambo ya nje wameashiria pia mkutano wa marais wa nchi mbili uliofanyika hivi karibuni pembeni ya kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya ya BRICS kilichofanyika mjini Johannesburg, Afrika Kusini, na wakakubaliana kuitisha kikao cha kamisheni ya pamoja ya Tehran na Dar es Salaam katika muda mfupi ujao.

Katika fremu ya kuwa na maingiliano yenye kujenga na ulimwengu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina mtazamo wa kuangalia upande mmoja tu wa nchi za Ulaya, bali inatilia mkazo kuimarisha uhusiano wake na mabara ya Afrika na Asia pia.

Soko kubwa la Afrika ni uwanja mwafaka kwa uuzaji wa bidhaa za Iran; na katika hali hiyo, bara hilo lina nafasi maalumu katika sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.../

 

Tags