Iran: Mapambano dhidi ya Israel yanaweza kuchukua mkondo mpana
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i103412-iran_mapambano_dhidi_ya_israel_yanaweza_kuchukua_mkondo_mpana
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ambayo yameutumbukiza Ukanda wa Gaza katika vita haribifu na vya kuogofya, huenda yakachukua mikondo mipya na mipana zaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 13, 2023 00:02 UTC
  • Iran: Mapambano dhidi ya Israel yanaweza kuchukua mkondo mpana

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ambayo yameutumbukiza Ukanda wa Gaza katika vita haribifu na vya kuogofya, huenda yakachukua mikondo mipya na mipana zaidi.

Hossein Amir-Abdollahian alitoa inadhari hiyo jana Alkhamisi akiwa Beirut, mji mkuu wa Lebanon, kikiwa ni kituo cha pili cha ziara yake ya kieneo, baada ya kuitembelea Iraq.

Amir-Abdollahian amesema, "Baadhi ya maafisa wa Ulaya wananiuliza iwapo kuna uwezekano wa kuibuka kambi mpya dhidi ya utawala wa Kizayuni? Nikawajibu kuwa, madhali Wazayuni wanaendeleza jinai zao za kivita, kuna uwezekano mkubwa wa harakati nyingine za mapambano (muqawama) zikajiunga na vita." 

Utawala haramu wa Kizayuni ulichukua uamuzi wa kuishambulia Gaza baada ya tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kutekeleza oparesheni Jumamosi iliyopita dhidi ya maghasibu wa Israel kwa jina la" Kimbunga cha al-Aqsa".

Amir-Abdollahian akiwa na maafisa wa Iraq kabla ya kuelekea Lebanon

Mashambulizi ya kikatili ya utawala haramu wa Israel dhidi ya raia wasio na ulinzi wa eneo la Ukanda wa Gaza linalokaliwa kwa mabavu yangali yanaendelea. Wapalestina zaidi ya 1,500 wameuawa shahidi mpaka sasa, mbali na wengine zaidi ya 6,000 kujeruhiwa, huku utawala katili wa Israel ukiendelea kuwashambulia kwa mabomu na makombora Wapalestina wa Gaza.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza kuwa, wananchi wa Palestina wana haki ya kisheria ya kujihami dhidi ya aina yoyote ya uchokozi na kukaliwa ardhi zao kwa mabavu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, "Tuko Beirut kutangaza kwa kinywa kipana kwamba, pamoja na nchi na serikali za Waislamu, tunapinga na kulaani vikali jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza."