Raisi: Inapasa kuwabebesha dhima wanaonyamazia kimya jinai za Israel
Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina ni katika misingi ya sera za Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa, wanaonyamazia kimya jinai za Israel watabeba mas'ulia mbele ya Mwenyezi Mungu, mienendo yao na historia.
Rais Raisi alisema hayo jana jioni katika kikao cha Baraza la Mawaziri hapa Tehran na kusisitiza kuwa, "Sera ya kikatili ya utawala wa Kizayuni ya kuwafurusha wakazi wa Gaza kutoka katika ardhi yao, ingawaje inapauuzwa, lakini inakanyaga sheria zote za kimataifa na misingi ya maadili na ubinadamu."
Sayyid Raisi amelaani vikali kimya cha serikali na jumuiya za kimataifa kwa jinai ambazo hazijawahi kushuhudiwa dhidi binadamu ambazo zinafanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina.
Utawala wa Kizayuni unaendeleza mashambulizi ya kikatili dhidi ya Ukanda wa Gaza, tangu baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) tarehe 7 mwezi huu wa Oktoba kutekeleza oparesheni kwa jina la "Kimbunga cha Al Aqsa" dhidi ya utawala huo ghasibu.
Mashambulizi hayo ya utawala wa Kizayuni katika maeneo ya raia katika Ukanda wa Gaza yamesababisha Wapalestina karibu 3,000 kuuawa shahidi na wengine zaidi ya 8,700 kujeruhiwa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametahadharisha kuwa, iwapo jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza hayazisitishwa, hali ya mambo itakuwa tete zaidi na yumkini vita hivyo vitaenea katika maeneo mengine.
Sayyid Raisi ameongeza kuwa, wanaomuamini Mwenyezi Mungu, na wana utu na wanaheshimu itibari ya historia, wanapasa kufahamu kuwa wamechangia jinai hizo (za Wazayuni) kwa ukimya wao, na wataenda kujibu mbele ya Mola Mtukufu.