Abdollahian alaani jinai za Israel Gaza: Muda wa utawala wa Kizayuni umemalizika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i103638-abdollahian_alaani_jinai_za_israel_gaza_muda_wa_utawala_wa_kizayuni_umemalizika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kitendo cha Israel cha kushambulia kwa mabomu hospitali na shule katika Ukanda wa Gaza huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kueleza kuwa: Muda wa kubaki hai utawala wa Kizayuni umemalizika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 18, 2023 08:55 UTC
  • Abdollahian alaani jinai za Israel Gaza: Muda wa utawala wa Kizayuni umemalizika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kitendo cha Israel cha kushambulia kwa mabomu hospitali na shule katika Ukanda wa Gaza huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kueleza kuwa: Muda wa kubaki hai utawala wa Kizayuni umemalizika.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo leo Jumatano katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter), akitoa radiamali yake kwa jinai ya kutisha ya Israel dhidi hospitali moja huko Gaza hapo jana.

Maghasibu wa Kizayuni jana usiku waliishambulia kwa mabomu hospitali ya Maamadani huko Gaza; na kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari Wapalestina 500 wameuliwa shahidi  katika jinai hiyo ya kinyama.

Amir-Abdollahian amesema: Baada ya utawala wa Israel kufanya mashambulizi ya kihaini na mauaji ya halaiki ya wanawake na watoto wasio na hatia wa Kipalestina katika Hospitali ya Al-Maamadani, wakati umefika kwa walimwengu kuungana kwa ajili ya ubinadamu dhidi ya utawala huu bandia, ambao unachukiwa zaidi ya ISIS, na ambao ni mashine ya mauaji. 

Amir-Abdollahian amekosoa vikali hatua ya jeshi katili la utawala wa Kizayuni ya kuendelea kushambulia nyumba na makazi ya raia huko Gaza kutokana na kushindwa kwenye medani za vita.

Maandamano ya kulaani jinai za kikatili za Wazayuni

Hadi sasa Wapalestina zaidi ya elfu 3 wameuawa shahidi na wengine elfu 12 na mia 500 kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Wazayuni huko Gaza tokea Oktoba 7.

Katika hatua nyingine, maelfu ya wananchi wa Iran wakiongozwa na madaktari, wauguzi na wahudumu wengine wa afya wamekusanyika katika Medani ya Palestina mjini Tehran, kulaani mashambulizi na jinai za utawala wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.

Katika maandamano hayo, wananchi wa Iran mbali na kutangaza mshikamano na Wapalestina, wameulaani utawala wa Kizayauni kwa hatua yake ya jana usiku ya kuipiga kwa mabomu Hospitali ya Maamadani huko Gaza na kuua shahidi mamia ya Wapalestina.