Amir Abdollahian: Utawala wa Kizayuni unafanya mauaji ya kimbari huko Gaza
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya mauaji ya kimbari huko Gaza.
Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, usiku wa kuamkia leo amehutubia kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Palestina kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, akizungumzia nafasi muhimu ya Iran katika kusaidia amani na utulivu na kupambana na ugaidi, na amezikosoa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya kwa kuunga mkono na kuukingia kifua utawala unaoukalia Quds kwa mabavu wa Israel. Amesema: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa kuhakikisha amani inakuwepo duniani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kuwa, Gaza inahitaji misaada ya dharura ya kibinadamu na kusema: Kwa mujibu wa sheria na maazimio ya kimataifa ya Baraza Kuu, wananchi wa Palestina wana haki halali ya kupambana dhidi ya uvamizi na kukaliwa kwa mabavu nchi yao.
Amir Abdollahian ameashiria kuwa, Marekani ndiyo sababu kuu ya kushindwa juhudi za kuweka wazi hatima ya wananchi wa Palestina na Baraza la Usalama.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesisitiza kwamba, ardhi ya Palestina ni mali ya wakazi wake wa asili wakiwemo Waislamu, Wakristo na Wayahudi, na kufafanua kuwa: Iran inaamini kwamba ni lazima kufanyike kura ya maoni kati ya watu wa asili wa Palestina ili kuweka wazi hatima yao kwa namna iliyorekodiwa katika Umoja wa Mataifa.
Akigusia uhalifu na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Magharibi mwa Asia, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema: Utawala huo umefanya jinai zote zikiwemo uvamizi, jinai dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari na haufuati sheria yoyote.
Ameitaja Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa kuwa ni jibu dhidi ya hujuma zinazoendelea kufanywa na Israel kwa wananchi wa Palestina na kukaliwa kwa mabavu nchi yao na kusema kuwa, ushiriki wa moja kwa moja wa Marekani katika mapigano hayo na misaada ya kifedha na kijeshi kwa utawala wa Israel ni ukiukaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran ametoa wito wa kuidhinishwa azimio kali katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kukomesha mara moja ukatili na mauaji ya kimbari ya raia na kutumwa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza.
Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Afya ya Palestina, zaidi ya watu 7,800 wameuawa shahidi na wengine takriban 20,000 wamejeruhiwa katika siku 20 za mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.