Iran yaiambia G7: Acheni kuunga mkono mauaji ya watoto Gaza
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewakosoa vikali Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Kundi la G7 kwa kutoa taarifa ya pamoja ya kuilaani Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina (Hamas) sambamba na kuunga mkono mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani taarifa hiyo ya G7 na kusisitiza kuwa haina msingi wowote.
Amesema inasikitisha kuona nchi hizo zilizostawi kiviwanda duniani za Marekani, Uingereza, Ujerumani, Italia, Canada, Ufaransa na Japan zinatoa taarifa ya kuinga mkono Israel licha ya utawala huo pandikizi kufanya kila aina ya jinai dhidi ya Wapalestina.
Kan'ani amesema uporaji wa ardhi za Palestina, mauaji ya halaiki na mauji ya kimbari, kushambulia maeneo ya makazi ya watu na mashamba, hujuma dhidi ya maeneo ya Kiislamu na kidini, kushambulia hospitali na vituo vya afya, kuua watoto wadogo na kuwadhalilisha Wapalaestina ni sehemu ndogo ya jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameeleza kuwa, inakatisha tamaa kuona wale wale ambao waliunda utawala bandia na kuunga mkono jinai za Wazayuni, ndio hao hao wanaoibua madai yasiyo na msingi ili kutaka kuonyesha kuwa makundi ya muqawama ndio yanayoyumbisha usalama na kuleta taharuki katika eneo.
Kan'ani amesisitiza kuwa, jinai zinazofanywa na Wazayuni katika Ukanda wa Gaza kuwa ni mauaji ya wazi ya kimbari. Mauaji hayo ya Israel katika Ukanda wa Gaza yamelaaniwa na shakhsia tofauti, jumuiya za kimataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Tangu Oktoba 7, utawala wa kibaguzi wa Israel umekuwa ukiendesha mauaji ya umati na ya kizazi dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza ambapo kufikia sasa umekwishaua bila huruma Wapalestina zaidi ya 10,600, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.