Mbunge Iran anusurika kuuawa na magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i11014-mbunge_iran_anusurika_kuuawa_na_magaidi
Mbunge mmoja nchini Iran amenusurika kuuawa katika hujuma ya kigaidi katika mkoa wa Kermanshah magharibi mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2016 23:09 UTC
  • Mbunge Iran anusurika kuuawa na magaidi

Mbunge mmoja nchini Iran amenusurika kuuawa katika hujuma ya kigaidi katika mkoa wa Kermanshah magharibi mwa nchi.

Duru zinaarifu kuwa gari lililokuwa limembeba Heshmatollah Falahatpishe, mwakilishi wa eneo la Eslamabad-e Gharb, alishambuliwa na magaidi wanne akiwa ndani ya gari katika kijiji cha Rijab siku ya Jumapili.

Taarifa zinasema mkuu wa wilaya ya Eslamabad-e Gharb, na mkurugenzi mkuu wa uvuvi Kermanshah, ambao pia walikuwa ndani ya gari hilo, walijeruhiwa lakini dereva na mkuu wa idara ya mifugo katika kata ya Dalahou walipoteza maisha katika ufyatuaji risasi huo.

Mbunge Falahatpishe hakupata majeraha makubwa katika hujuma hiyo na tayari maafisa wa usalama wameshaanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Imearifiwa kuwa, magaidi waliotekeleza hujuma hiyo waliteketeza moto gari walilokuwa wakilitumia kabla ya kutoroka. Makundi ya magaidi wanaopata himaya ya maadui wa Iran wamekuwa wakitekeleza mashambulizi katika maeneo ya mipakani katika miezi ya hivi karibuni kwa lengo la kuvuruga usalama nchini.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC mwezi Juni liliangamzia magaidi watano katika eneo la kaskazini magharibi mwa nchi karibu na mpaka wa Uturuki.

Magaidi walioangamizwa walikuwa wa kundi la PJAK. Kundi hilo lilibuniwa miaka 13 iliyopita na kundi jingine la Kurdistan Workers' Party PKK lililo na makao yake nchini Uturuki na katika eneo la Kurdestan la kaskazini mwa Iraq kwa lengo la kutekeleza hujuma za kigaidi katika eneo la magharibi mwa Asia na ndani ya Iran.