Apr 16, 2024 07:08 UTC
  • Abdollahian amwambia Guterres: Hatukuwa na njia nyingine isipokuwa kuiadhibu Israel

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa, operesheni ya jeshi la Iran dhidi ya maeneo ya kijeshi ya utawala ghasibu wa Israel imefanyika ndani ya fremu ya kujilinda na kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdollahian, ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na kuongeza kuwa, kutokana na utepetevu wa Baraza la Usalama na kushindwa kwake kulaani mashambulizi utawala wa Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, kujilinda kihalali na kuuadhibu utawala wa Kizayuni wa Israel lilikuwa chaguo pekee la Iran la kukabiliana na mchokozi.

Akielezea kuwa operesheni ya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Israel imefanyika katika fremu ya haki halali ya kujilinda na kwa mujibu wa sheria za kimataifa, Amir Abdollahian ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran licha ya kuwa na uwezo wa kutekeleza operesheni kubwa na pana zaidi, lakini ililenga tu sehemu na maeneo ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni, yaliyotumiwa  kushambulia ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus.

Amir Abdollahian

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amepongeza juhudi binafsi za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kuwasaidia wananchi wa Palestina na kusema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukiwaua watoto na wanawake wasio na ulinzi na kufanya mauaji ya kimbari kwa muda wa miezi sita huko Gaza; na Marekani na washirika wake hawasimamishi mauaji ya kimbari ya utawala huo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amezungumzia pia oparesheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na kutoa wito wa kuendelezwa hali ya kujizuia pande zinazohusika katika migogoro wa eneo la Magharibi mwa Asia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani mashambulizi dhidi ya maeneo ya kidiplomasia na amepongeza msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kusimamisha hujuma zaidi dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Tags