Apr 17, 2024 02:28 UTC
  • Rafael Grossi
    Rafael Grossi

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA amesisitiza kuwa, hakuna nyaraka zozote zinazothibitisha utengenezaji wa silaha za nyuklia nchini Iran na kuwa, mivutano ya hivi sasa haijavuruga mchakato wa ufuatiliaji wa wakala huo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Katika kujibu swali kuhusu matukio mapya katika mpango wa nyuklia wa Iran, Grossi amekariri baadhi ya madai ya kisiasa na kusema: "Iran inahifadhi kiwango kikubwa sana cha urani iliyorutubishwa lakini hii haina maana kuwa ina silaha za nyuklia. Ameongeza kuwa: "Bila shaka kwa upande wa Shirika la IAEA  ni lazima tuwe waangalifu tunapotoa habari kwa ujumla na hatuna taarifa yoyote au dalili zinazothibitisha kwamba Iran ina mpango wa kuzalisha silaha za nyuklia." Grossi ameongeza kuwa, tumeutaarifu upande wa Iran kwamba kiwango hiki cha akiba ya urani, ambacho kitaalamu kinakaribia kiwango kinachohitajika kwa ajili ya kutengeneza silaha za nyuklia, kinatia shaka na wasiwasi katika ngazi za kimataifa, na kwa sababu hiyo, tumewataka washirikiane na sisi kikamilifu. Grossi ameelezea matumaini kwamba ataweza kusafiri mjini Tehran katika kipindi cha wiki chache zijazo na kutoa taarifa kuhusiana na jambo hilo.

Kuthibitisha tena Grossi kwamba Iran haijishughulishi na mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia kwa mara nyingine tena kumethibitisha kutokuwa na msingi wowote madai ya mara kwa mara ya Marekani na utawala wa Kizayuni, pamoja na baadhi ya washirika wa Washington wa Ulaya na Troika ya Ulaya, kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran unaotekelezwa kwa malengo ya amani.

Kwa hakika madai ya uwongo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran ni madai ambayo yamekuwa yakikanushwa mara kwa mara na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), na  kusisitiza kwamba mpango wa nyuklia wa Iran ni wa amani. Suala hilo limethibitishwa katika ripoti zake nyingi zinazotolewa kimataifa. Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki,  katikati ya Novemba 2022 alisema kwamba: "Hatuna taarifa zozote zinazothibitisha kwamba hivi sasa Iran inazalisha silaha za nyuklia.

Makao makuu ya IAEA mjini Vienna Austria

 Kauli za Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuhusu kutokuwepo mpango wa kijeshi wa nyuklia nchini Iran zinatolewa katika hali ambayo  Wamagharibi wanatekeleza siasa za kuishinikiza Iran kupitia wakala huo na pamoja na mambo mengine kupitisha maazimio dhidi ya mpango wa amani wa Iran katika bodi ya magavana wa wakala huo.

Ingawa maendeleo ya nyuklia ya Iran yanawiana na malengo ya amani, lakini Marekani, washirika wake wa Magharibi na utawala wa Kizayuni wanayatumia kama kisingizio cha kuituhumu Tehran kuwa inafuatilia malengo ya kijeshi. Tuhuma hizo zimekaririwa mara nyingi katika nyaraka muhimu za Marekani.

Kwa miaka mingi, Wamagharibi wameishutumu Iran kuwa ina mpango wa kijeshi wa nyuklia, licha ya kutotoa ushahidi wowote kuhusiana na suala hili, na wamechukua hatua nyingi za kisiasa na vikwazo dhidi ya Iran kwa kisingizio hicho hicho. Msemaji wa Ikulu ya White House Karin Jean-Pierre alidai mnamo Agosti 2022 kuwa: "Rais Biden amethibitisha kwamba anataka kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia." Shutuma hizi zinatolewa huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikitangaza mara kwa mara kwamba sio tu kwamba haina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia, bali hata haina nia ya kuelekea huko. Kwa hakika, shutuma za Washington dhidi ya Tehran zinatokana na hofu yake kuhusu kuimarika nguvu za Iran katika nyanja mbalimbali.

Kwa hakika, kinyume na tuhuma zisizo na msingi za nchi za Magharibi kuwa Tehran inataka kutengeneza silaha za nyuklia, Iran imeweza kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani katika nyanja mbalimbali zikiwemo za uzalishaji umeme, dawa, kilimo na sekta nyinginezo. Ni wazi kuwa suala ambalo linaitia wasiwasi mkubwa Marekani na waitifaki wake wa Ulaya na vilevile utawala wa Kizayuni ni kuongezeka nguvu ya Iran kuhusu suala zima la matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.

 

Tags