Jul 15, 2016 16:07 UTC
  • Ayatullah Kashani: Marekani, Saudia na Israel ni waungaji mkono wakubwa wa ugaidi

Hatibu wa Swala ya Ijumaa hapa Tehran amesema kuwa Marekani, Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel ni waungaji mkono wakubwa wa ugaidi duniani.

Akizungumza katika hotuba za Swala ya Ijumaa hii leo hapa Tehran, Ayatullah Muhammad Emami Kashani ameashiria hali mbaya inayotawala katika nchi za eneo Mashariki ya Kati na mauaji ya raia wasio na hatia yanayoendelea katika nchi hizo na kueleza kuwa: Kuanzisha makundi ya kigaidi kwa lengo la kuwaangamiza raia na miundo mbinu ya nchi kama Iraq, Syria na Yemen ni jinai ya wazi wazi dhidi ya ubinadamu.

Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo katika jiji la Tehran amesema kuwa Marekani inadai kutetea haki za binadamu duniani huku nchi hiyo ikiendelea kuwaunga mkono maadui wa mataifa madhulumu ya Iraq, Syria na Yemen na kunyamaza kimya mbele ya jinai zinazofanywa na matakfiri na Mawahabi katika nchi hizo.

Ayatullah Emami Kashani ameashiria pia uvamizi na uchokozi wa utawala wa Kizayuni huko Palestina na kusema: Marekani na baadhi ya nchi waitifaki wake wa Magharibi wanawatuhumu wananchi wa Palestina kuwa ni magaidi; raia ambao hawafanyi lolote ghairi ya mapambano na kutetea haki na ardhi zao zilizoghusubiwa.

Imamu wa Swala ya Ijumaa ya leo hapa Tehran pia amesema anatiwa wasiwasi na hali mbaya inayowakabili wananchi wa Yemen na kulaani mashambulizi ya utawala wa Aal Saudi nchini humo. Ayatullah Kasheni amesema nchi ya Yemen ni ya Wayemeni wenyewe na kwamba hakuna mtu aliye na haki ya kuainisha mustakbali wa nchi hiyo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Emami Kashani ameashiria madai ya baadhi ya viongozi wa Magharibi ya kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inaunga mkono ugaidi na kueleza kuwa, nchi zote duniani zimeshuhudia kuwa kundi la kigaidi la Daesh linaendeshwa kwa nguvu za Marekani, pesa za utawala wa Aal Saud na siasa za Wazayuni. Khatibu wa Swala ya Ijumaa hapa Tehran amesema anataraji kuwa nchi za eneo hili na zile za Kiislamu hususan Bahrain, Iraq, Syria na Yemen zitapata amani na utulivu.

Tags