Jun 27, 2024 03:00 UTC
  • Ghazizadeh Hashemi ajiondoa katika kinyang'anyiro cha urais wa Iran

Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi, mmoja wa wagombea sita wa kiti cha rais ajaye wa Iran, amejiondoa katika kinyang'anyiro hicho. Uchaguzi huo wa kabla ya wakati wake unafanyika kesho Ijumaa tarehe 28 Juni, 2024.

Hashemi, ambaye ni mbunge wa zamani na ni makamu wa zamani wa rais, ametangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho katika taarifa yake ya jana Jumatano.

Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi, ambaye kwa sasa anahudumu kama mkuu wa Wakfu wa Mashahidi na Masuala ya Veterani, ametaja sababu ya yeye kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho kuwa ni kutetea urithi wa rais wa zamani Ebrahim Raisi, ambaye alikufa shahidi katika ajali ya helikopta tarehe 19 mwezi uliopita wa Mei 19 akiwa pamoja na wasaidizi wake kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Amir-Abdollahian. 

Kupitia taarifa yake, Hashemi alisema anajivunia kupata nafasi ya kufanya kazi pamoja na Rais Raisi. Pia amesema hakuacha kufanya juhudi yoyote ya kutetea rekodi ya utendaji ya shahid Raisi wakati wa kampeni za uchaguzi huu.

Ghazizadeh Hashemi (katikati) ametangaza kujitoa kwenye kinyang'anyiro cha urais wa Iran

 

Vile vile amesema kuwa, Iran lazima ilipe umuhimu suala la kufanya kazi na mataifa jirani na yale ambayo hayakubali kuburuzwa na Marekani.

Pia ameahidi kuendeleza sera ya kimkakati ya uhusiano wa kimataifa aliyokuwa akiiendesha Rais Raisi kwani amesema imezaa mafanikio mengi.

Wagombea waliosalia kwenye kinyang'anyiro hicho ni watano, Saeed Jalili, aliyewahi kuwa mkuu wa timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran, Mostafa Pourmohammadi, waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Masoud Pezeshkian, waziri wa zamani wa afya na Alireza Zakani, meya wa jiji la Tehran.