Ayatullah Khamenei: Kipaumbele muhimu ni utekelezaji wa makubaliano kati ya Iran na Iraq
(last modified 2024-07-31T03:36:55+00:00 )
Jul 31, 2024 03:36 UTC
  • Ayatullah Khamenei: Kipaumbele muhimu ni utekelezaji wa makubaliano kati ya Iran na Iraq

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Iraq kwamba utekelezwaji wa mapatano baina ya nchi hizo mbili ndio kipaumbele muhimu zaidi.

Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo jioni ya jana akiwa katika kikao na Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia Al-Sudani na ujumbe aliofuatana nao mjini Tehran. Aliashiria hati zilizotiwa saini kati ya Iran na Iraq katika kipindi cha serikali ya Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi na kusisitiza haja ya kufuatiliwa mikataba hiyo na utekelezaji wake katika kipindi kipya. Ameongeza kuwa: Kasi ya utekelezaji wa mikataba ya nchi mbili inapaswa kuzidishwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza kufurahishwa kwake na hatua za serikali ya Mohammad Shia Al-Sudani za kutatua matatizo ya Iraq na kueleza kuridhishwa kwake na uratibu na ushirikiano uliopo kati ya mikondo mbalimbali ya kisiasa ya Iraq. Amesema kuna ulazima wa kuendelezwa ushirikiano huo.

Ayatullah Khamenei, ametoa shukrani kwa juhudi na jitihada za wananchi na serikali ya Iraq kwa ajili ya kufanyika vyema matembezi adhimu ya makumi ya mamilioni ya Arubaini ya Imam Hussein (as), na amesisitiza kuwa kufuatilia mafaili ya makubaliano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq na kuyakamilisha ni moja ya vipaumbele vya uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika kipindi hiki kipya.

Ayatullah Khamenei na Mohammad Shia Al-Sudani 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria ripoti ya Waziri Mkuu wa Iraq kuhusu maandalizi yaliyofanywa kwa ajili ya matembezi salama na yenye amani ya Arubaini ya Imam Hussein na kusema: Mapokezi makubwa ya wananchi wa Iraq ya idadi kubwa ya Waislamu wanaomzuru Imam Hussein (as), pamoja na hatua zilizochukuliwa na serikali ya Iraq ili kuhakikisha usalama wa tukio hili kubwa ni jambo muhimu sana na la kushangaza.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Iraq amepongeza kufanyika kwa mafanikio uchaguzi wa rais wa Iran na kueleza matumaini yake kuwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Iran na Iraq yatatekelezwa katika kipindi hiki kipya.

Mohammad Shia al-Sudani amepongeza misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kusema: "Utawala wa Kizayuni wa Israel umevuka mipaka yote ya kimataifa na ya kibinadamu, na msimamo wa umma na rasmi wa Iraq kuhusu uhalifu huo uko thabiti na endelevu, na serikali ya Baghdad inaendeleza mawasiliano na nchi ambazo zina msimamo wa pamoja.

Akizungumzia matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein yanayofanyika kila mwaka siku ya arubaini baada ya tarehe 10 Muharram, Waziri Mkuu wa Iraq amesema, shughuli hiyo kubwa ni fursa ya kuchukua misimamo dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni na kuwafahamisha Waislamu, hususan vijana, misingi na mafundisho ya mapambano ya Imam Hussein dhidi ya madhalimu.

Tags