Kan'ani: Wahalifu wa Tel Aviv ni wafyonza damu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria mauaji ya muigizaji maarufu wa Kipalestina yaliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel na kusema kuwa, damu ya Rashad abu Skheileh na zaidi ya Wapalestina wengine 40,000 wa Ukanda wa Gaza ni ithibati ya roho chafu na ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Nasser Kan'ani amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kueleza kuwa, "Damu ya Wapalestina inalia jinsi Wapalestina wanavyokandamizwa na jinsi wale wanaojiita watetezi wa haki za binadamu wanavyoongopa."
Kan'ani ameeleza bayana kuwa, jinai za Wazayuni zimeshtadi na kuongezeka hasa katika Ukanda wa Gaza; huku kundi la wahalifu huko Tel Aviv likifyonza damu ya binadamu kama jinamizi.
Katika muendelezo wa jinai zake za hivi punde dhidi ya Wapalestina, utawala ghasibu wa Israel umemuua Rashad abu Skheileh baada ya kushambulia kwa mabomu skuli katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia huko Gaza.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa wito wa kuwajibishwa viongozi watenda jinai wa utawala wa Israel kwa jinai zao dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.
Kan'ani ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka ili kuizuia Israel kufanya uhalifu zaidi dhidi ya Wapalestina wasio na hatia.
Wapalestina zadi ya 40,700 wameuawa shahidi na wengine zaidi ya laki moja wamejeruhiwa katika mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanya na Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.