Rais Pezeshkian wa Iran kuitembelea Iraq katika ziara ya kwanza nje ya nchi
(last modified 2024-09-08T11:35:53+00:00 )
Sep 08, 2024 11:35 UTC
  • Rais Pezeshkian wa Iran kuitembelea Iraq katika ziara ya kwanza nje ya nchi

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian anatazamiwa kuitembelea Iraq siku ya Jumatano katika safari yake ya kwanza ya nje tangu aingie madarakani.

Rais ameratibiwa kukutana na maafisa wakuu wa Iraq na kutia saini hati za ushirikiano na usalama, katika fremu ya sera za Jamhuri ya Kiislamu za kupanua uhusiano na nchi marafiki na majirani.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran (IRNA), hii itakuwa ziara ya kwanza ya Rais Pezeshkian nje ya nchi tangu achukue hatamu za uongozi mwishoni mwa Julai mwaka huu.

Katika ziara yake hiyo, Rais wa Iran anatazamiwa kufanya mazungumzo na viongozi wenzake, kuhudhuria vikao vya wajumbe wa ngazi za juu, kushiriki katika mikutano na waandishi wa habari na kutia saini hati kadhaa za ushirikiano.

Tarehe 28 Agosti, Balozi wa Iran mjini Baghdad, Mohammad Kazem Al-e-Sadeq alitangaza ziara ya Rais Pezeshkian wakati wa mahojiano na shirika la habari la IRNA.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran alisema kuwa Dakta Pezeshkian ataelekea katika nchi hiyo ya Kiarabu, kuitikia mwaliko rasmi wa Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia’ Al Sudani.

Rais Pezeshkian amekuwa akisisitiza kuwa, serikali yake itatoa kipaumbele kwa uhusiano na nchi jirani pamoja na mataifa rafiki ambayo yameiunga mkono Iran katika nyakati ngumu.

Tags