Rais wa Iran na Waziri Mkuu wa Iraq wafanya mkutano na waandishi wa habari Baghdad
(last modified 2024-09-12T03:11:51+00:00 )
Sep 12, 2024 03:11 UTC
  • Rais wa Iran na Waziri Mkuu wa Iraq wafanya mkutano na waandishi wa habari Baghdad

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Iraq: "tunapaswa kutekeleza makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama kati ya Iran na Iraq ili kukabiliana na magaidi na maadui".

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB Rais Masoud Pezeshkian amesema katika mkutano huo aliofanya na waandishi wa habari jana Jumatano akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Iraq Mohammad Shia al-Sudani: "tunahitaji kutekeleza makubaliano ya ushirikiano wa kiusalama kati ya nchi mbili ili kukabiliana na magaidi na maadui, ambao huko nyuma waliulenga uthabiti na usalama wa eneo".
 
Akizungumzia mikutano iliyofana aliyofanya na Waziri Mkuu na Rais wa Iraq, Pezeshkian alisema: Hati 14 za makubaliano ya ushirikiano zimetiwa saini kati ya Iran na Iraq, ukiwa ni mwanzo wa kupanuliwa ushirikiano kati ya nchi mbili.
 
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza pia kwamba, wamezungumzia hali ya kijiografia ya nchi mbili na akasema: Iran na Iraq ni nukta zinazounganisha Ulaya na Asia.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Iraq wakibadilishana hati za maelewano

Pande hizo pia zimejadili kuunda kundi la wataalamu wa fani hii na mipango mkakati na ya muda mrefu itakayoleta ushirikiano mkubwa kati ya nchi hizo mbili.

 
Katika mkutano huo na waandishi wa habari,  Pezeshkian amezungumzia pia masuala ya eneo na akaeleza kwamba: sura halisi ya utawala muuaji wa Kizayuni unaofanya mauaji ya kimbari Ghaza na za serikali zinazouunga mkono utawala huo zikidai kuwa watetezi wa haki za binadamu zimedhihirika wazi; na jinai za utawala huo ghasibu zimedhihirisha kwa wazi kabisa madai ya uwongo ya nchi za Magharibi na jumuiya za kimataifa kuhusu haki za binadamu.
 
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia al-Sudani alisema: "uhusiano wa Iran na Iraq ni wa kina na wa muda mrefu na unaendelea katika nyuga tofauti, na ujirani mwema uliopo baina nchi hizo mbili unaweza kuwa njia ya kupanua uhusiano kati ya pande mbili.
 
Aidha, Waziri Mkuu wa Iraq amewashukuru ndugu zake wa Iran kwa ushiriki wao katika mapatano ya ushirikiano wa gesi kati ya Turkmenistan na Iraq na akasema: "tumesisitiza mara kadhaa kwamba tunapinga kupanuliwa wigo wa mivutano na migogoro dhidi ya mamlaka ya nchi, na kuna umuhimu kwa jamii ya kimataifa kutimiza wajibu na jukumu lake la kisheria na kimaadili".../
 
 

 

Tags