Rais wa Iran awasili eneo la Kurdistan la Iraq katika siku ya pili ya ziara yake nchini humo
(last modified 2024-09-12T07:41:15+00:00 )
Sep 12, 2024 07:41 UTC
  • Rais wa Iran awasili eneo la Kurdistan la Iraq katika siku ya pili ya ziara yake nchini humo

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili katika eneo la Kurdistan la Iraq katika siku ya pili ya ziara yake ya kuitembelea nchi hiyo.

Kwa mujibu wa IRNA, Rais Pezeshkian amewasili katika eneo la Kurdistan leo Alkhamisi katika siku ya pili ya safari yake nchini Iraq, na kukaribishwa na rais wa eneo hilo, Nichervan Barzani.
 
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye jana (Jumatano) alisafiri kuelekea Iraq kwa ziara ya siku tatu, amesema katika mahojiano na kanali ya habari ya Rudaw kwamba uhusiano kati ya Iran na eneo la Kurdistan hivi sasa ni mzuri na juhudi zinapasa kufanywa ili kuimarisha zaidi uhusiano huo.
Rais Pezeshkian (kushoto) na mwenyeji wake Waziri Mkuu Mohammad Shia al-Sudani

Jana Jumatano, Rais Pezeshkian alielekea nchini Iraq huku akiongozana na ujumbe wa ngazi za juu wa maafisa wa kisiasa na kiuchumi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kulakiwa na kukaribishwa rasmi na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mohammad Shia al-Sudani alipowasili katika uwanja wa ndege wa Baghdad.

 
Rais wa Iran vilevile alifanya mazungumzo na Rais na Waziri Mkuu wa Iraq katika vikao tofauti.
 
Halikadhalika, hati 14 za ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kibiashara, kiutamaduni na kijamii zilitiwa saini na maafisa wa nchi hizo mbili katika hafla iliyohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia al-Sudani.../

 

Tags