Araghchi: Ushindi Wa Muqawama unasimulia mafanikio yake na kushindwa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i122328-araghchi_ushindi_wa_muqawama_unasimulia_mafanikio_yake_na_kushindwa_israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi ameashiria umuhimu wa kusimuliwa kwa usahihi mafanikio ya Mrengo wa Muqawama wa Palestina katika kupinga jinai za Israel.
(last modified 2025-02-04T23:12:22+00:00 )
Feb 04, 2025 23:12 UTC
  • Araghchi: Ushindi Wa Muqawama unasimulia mafanikio yake na kushindwa Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi ameashiria umuhimu wa kusimuliwa kwa usahihi mafanikio ya Mrengo wa Muqawama wa Palestina katika kupinga jinai za Israel.

Araghchi amesema hayo akihutubia Kongamano la Kimataifa kuhusu Gaza na Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, lililofikia tamati jana Jumanne hapa mjini Tehran, ambapo amesisitiza haja ya kuakisiwa kwa usahihi mafanikio ya Harakati ya Muqawama ya Hamas mkabala wa utawala wa Kizayuni katika vita dhidi ya Gaza.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema, "Medani na diplomasia si nyanja tofauti, bali ni seti iliyounganishwa. Diplomasia inakuza mafanikio ya medani na kuyabadilisha kuwa maslahi na mafanikio ya kitaifa."

Araghchi amesema Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ya tarehe 7 Oktoba 2023, iliashiria hatua ya mabadiliko katika historia ya sasa ya Palestina na eneo pana la Asia Magharibi.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amebainisha kuwa, operesheni hiyo iliyotekelezwa kwa upangaji wa kina na usahihi mkubwa na Muqawama wa Wapalestina dhidi ya uvamizi wa Israel, iliifanya jamii ya kimataifa kutathmini upya msimamo wake kuhusu suala la Palestina, amani ya eneo, kufanya wa kawaida uhusiano na Israel, na kuanzishwa kwa taifa la Palestina.

Duru ya Kwanza ya Mkutano wa Kimataifa wa “Kimbunga cha al-Aqsa na Gaza; Simulizi na Uhalisia” ilihitimishwa jana Jumanne katika bewa la Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad cha Tehran.