Spika Ghalibaf: Iran inaunga mkono uthabiti nchini Sudan
(last modified Tue, 18 Feb 2025 07:38:10 GMT )
Feb 18, 2025 07:38 UTC
  • Spika Ghalibaf: Iran inaunga mkono uthabiti nchini Sudan

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad Baqer Ghalibaf amesema Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono juhudi za kurejeshwa utulivu na uthabiti nchini Sudan, sanjari na kuundwa "utawala wa umoja" ambao utahakikisha kuwa taifa hilo lina mamlaka kamili ya kujitawala.

Katika kikao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ali Youssef Ahmed al-Sharif hapa mjini Tehran jana Jumatatu, Ghalibaf ameonya dhidi ya njama mpya za maadui na kuitaka nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kubuni mipango kabambe ya kuzima njama hizo.

Spika Ghalibaf amebainisha kuwa: Iran inaamini kuwa, ili kukabiliana na njama hizo ni lazima kwanza tufahamu kuwa utawala wa Israel ni adui nambari moja wa nchi za Kiislamu na nchi za eneo hili.

Ameeleza azma ya Iran ya kupanua uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara na Sudan na kubainisha kwamba, ziara ya hivi sasa ya mwanadiplomasia huyo mkuu wa Sudan mjini Tehran ni hatua chanya katika kufanikisha suala hilo.

Aidha Spika wa Bunge la Iran ameeleza kuwa, Bunge la Jamhuri ya Kiislamu liko tayari kuanzisha uhusiano wa kibunge na Sudan mara tu litakapoundwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, (kushoto) amekutana pia na mwenzake wa Iran, Abbas Aragchi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan kwa upande wake, amesema nchi yake imekuwa katika hali ngumu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na inakabiliwa na njama za kimataifa ambazo zinalenga kuligawanya taifa hilo na kupora rasilimali zake.

Sharif ameipongeza Iran kwa kuungana mkono jitihada za kurejeshwa utulivu na mamlaka ya kujitawala nchini Sudan na kuongeza kuwa, Wasudan milioni mbili waliokimbia makazi yao wanaishi katika nchi jirani, mbali na makumi ya maelfu ya watu wakiwemo wanawake, wanaume na watoto kuuawa.