Iran yamjibu Zelensky; yamwambia dunia imechoka na 'vikaragosi vilivyochanganyikiwa'
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135830-iran_yamjibu_zelensky_yamwambia_dunia_imechoka_na_'vikaragosi_vilivyochanganyikiwa'
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amemkosoa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kwa kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu, na kumwambia bayana kwamba dunia imechoka na "Wanaserere Waliochanganyikiwa."
(last modified 2026-01-24T03:32:49+00:00 )
Jan 24, 2026 03:32 UTC
  • Iran yamjibu Zelensky; yamwambia dunia imechoka na 'vikaragosi vilivyochanganyikiwa'

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amemkosoa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kwa kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu, na kumwambia bayana kwamba dunia imechoka na "Wanaserere Waliochanganyikiwa."

Araghchi amesema hayo akijibu matamshi ya Zelensky dhidi ya Iran wakati wa hotuba yake katika Jukwaa la Uchumi Duniani la Davos nchini Uswisi.

Waziri Araghchi amesema katika ujumbe alioutuma kwenye akaunti yake ya X jana Ijumaa kuwa, "Zelensky amekuwa akiwakomba walipa kodi wa Marekani na Ulaya ili kujaza mifuko ya majenerali wake mafisadi na kukabiliana na kile anachokiita uchokozi haramu unaokiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa."

Araghchi ameeleza kuwa, "(Zelensky) Wakati huo huo, anatoa wito waziwazi na bila aibu wa uvamizi haramu wa Marekani dhidi ya Iran kinyume na Mkataba huo huo wa Umoja wa Mataifa."

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran huku akimhutubu Rais wa Ukraine ameeleza bayana kuwa, "Dunia imechoka na Wanasesere Waliochanganyikiwa, Bwana Zelensky."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemtanabahisha Zelensky kwa kumwambia kuwa: Tofauti na jeshi lako linaloungwa mkono na maajinabii na lililojaa mamluki, sisi Wairani tunajua jinsi ya kujilinda na hatuna haja ya kuwaomba wageni msaada.

Matamshi ya Araghchi yamekuja baada ya Zelensky kubwabwaja wakati akihutubia mkutano wa Davos nchini Uswisi na kudai kwamba, kutochukua hatua dunia dhidi ya Iran kunachochea ongezeko la vitisho vya usalama.