Araghchi: Iran inaingia kwenye mazungumzo 'ikiwa makini'
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesema Tehran inaingia katika duru mpya ya mazungmzo ya kidiplomasia na Marekani ikiwa hadhiri, makini kabisa na "kwa macho yaliyo wazi."
Araghchi amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X leo Ijumaa, saa chache baada ya kuwasili Oman, akisisitiza kuwa Tehran inashiriki mazungumzo hayo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani mjini Muscat, ikiwa na nia na irada njema, huku ikitetea kwa uthabiti haki za taifa la Iran.
Waziri Araghchi amesisitiza kwamba, Iran ina "kumbukumbu thabiti ya mwaka uliopita" katika mazungumzo, akiashiria tahadhari iliyochochewa na uzoefu wa huko nyuma. Huku akisisitiza utayarifu wa Iran wa kufungamana na diplomasia, ameeleza bayana kwamba, Tehran "itasimama kidete kutetea haki zake."
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran aidha amesisitiza kwamba, kujenga hali ya kuaminiana kunategemea vitendo, na wala sio maneno matupu, akibainisha kuwa "ahadi zinazotolewa zinapasa kuheshimiwa."
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameongeza kuwa, kanuni kama vile "mazingira sawia," "heshima kwa pande zote," na "maslahi ya pande zote" si misimamo ya kauli tu, bali ni msingi muhimu wa kufikiwa makubaliano yoyote ya kudumu, akisitiza msimamo wa Iran kwamba diplomasia endelevu inahitaji usawa na mlingano.
Kama ilivyotangazwa hapo awali na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani inafanyika leo mjini Muscat kwa upatanishi wa Oman.
Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, Steve Witkoff, Mjumbe Maalum wa Rais wa Marekani kwa eneo la Asia Magharibi, na Jared Kushner, mkwe na msaidizi wa Donald Trump, wataiwakilisha Washington katika mazungumzo na Iran. Witkoff aliwasili Muscat saa chache kabla ya ujumbe wa Iran ukiongozwa na Waziri Araghchi kuwasili.