Qalibaf: Hali ya Hormuz haitarudi tena kama ilivyokuwa zamani
-
Mohammad Bagher Qalibaf
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unalenga kutumia vita kubadilisha muundo wa eneo la Asia ya Magharibi.
Mohammad Bagher Qalibaf amesisitiza kwamba: “Sura na mpangilio wa eneo utabadilika, lakini hautakuwa ule unaotawaliwa na matakwa ya Wazayuni na Marekani.”
Qalibaf alikumbusha kwamba utawala wa kiimla wa Pahlavi uliokuwa ukitawala Iran kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 ulikuwa kama askari wa kulinda maslahi ya Magharibi katika eneo la Asia Magharibi na ulitoa huduma kamili kwa utawala wa Kizayuni na Marekani.
Hata hivyo Mapinduzi ya Kiislamu yalivunja mnyororo huo na kuvuruga mpangilio huo wa zamani. Qalibaf amekumbusha kauli ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) aliyewahi kusema kwa maana hii: “Marekani, mnafanya nini hapa?” ambapo Wamarekani walidai kuwa wana maslahi katika eneo hilo. Kwa mujibu wa Qalibaf, Imam alijibu: “Hamna haki ya kudai maslahi katika eneo letu; maslahi haya ni ya watu wetu.”
Ameongeza kuwa Marekani imekuwa ikipora utajiri wa eneo hili bila kuleta usalama, bali kinyume chake imevuruga usalama wa eneo.
Akizungumzia Lango Bahari la Hormuz, Qalibaf amesema: “Ikiwa leo Lango Bahari la Hormuz limefungwa, si kwa sababu ya nia au uamuzi wetu wa kufunga, bali ni matokeo ya wajibu wetu wa kujilinda.” Amefafanua kwamba Iran haikuwa na nia ya kuyashambulia mataifa jirani, lakini akauliza ikiwa ni sahihi kutojibu wakati adui anarusha makombora au ndege kuelekea Iran kutoka maeneo ya nchi nyingine. Amesisitiza kuwa ni haki ya kisheria ya Iran kujilinda.
Ameongeza kuwa kwa sasa meli nyingi zimepunguza au kusitisha safari zao kwa sababu mazingira ya usalama hayaruhusu. Kwa maoni yake, kutokana na hali ya sasa na uingiliaji uliotokea, kisheria na kiusalama, lango hilo muhimu la bahari halitaweza kurudi katika hali ya awali ya usafiri wa baharini.
Qalibaf pia ameashiria kauli za viongozi wa utawala wa Kizayuni waliodai kwamba vita vitaubadilisha muundo wa Asia ya Magharibi. Amesema mabadiliko yanaweza kutokea, lakini hayatakuwa kwa msingi wa matakwa ya Marekani; badala yake, yatategemea mpangilio wa kikanda unaoundwa na nchi za eneo zenyewe.
Amesisitiza kuwa Iran ina mahusiano ya ujirani na ushirikiano wa kiuchumi na kiusalama na mataifa mengi ya eneo hilo, na kupitia ushirikiano wa pande mbili na wa pande nyingi, nchi za eneo hilo zina uwezo wa kujenga mfumo wa usalama wa kikanda bila kuingiliwa na madola ajinabi.