Iran yazitaka nchi za Kiislamu zitangaze msimamo, yasema Marekani haiaminiki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137416-iran_yazitaka_nchi_za_kiislamu_zitangaze_msimamo_yasema_marekani_haiaminiki
Katika taarifa yenye vipengele sita iliyoelekezwa kwa serikali za nchi za Kiislamu, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema: “Lazima muamue msimamo wenu katika Vita vya Ramadhani, je, mnasimama upande wa nchi ya Kiislamu ya Iran, au upande wa Marekani na Israel?”
(last modified 2026-03-17T07:35:17+00:00 )
Mar 17, 2026 04:45 UTC
  • Ali Larijani
    Ali Larijani

Katika taarifa yenye vipengele sita iliyoelekezwa kwa serikali za nchi za Kiislamu, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema: “Lazima muamue msimamo wenu katika Vita vya Ramadhani, je, mnasimama upande wa nchi ya Kiislamu ya Iran, au upande wa Marekani na Israel?”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, alitoa taarifa hiyo siku ya Jumatatu ambapo amezihutubu serikali za Kiislamu, kwa kuandika:

“Iran imekabiliwa na uchokozi wa hila wa Marekani na Uzayuni; uchokozi uliotokea wakati wa mazungumzo na uliolenga kuivunja na kuisambaratisha nchi, na kusababisha kuuawa shahidi kwa viongozi wa kujitolea wa Mapinduzi ya Kiislamu, pamoja na raia wa kawaida na makamanda wa kijeshi. Uchokozi huo umekabiliwa na  mapambano ya kitaifa na  muqawama wa Kiislamu kutoka kwa wananchi wa Iran.”

Taarifa hiyo inaongeza: “Mnajua vyema kwamba, isipokuwa katika hali chache sana, na hata hizo zikiwa zaidi za kisiasa, hakuna serikali ya nchi ya Kiislamu iliyokuja kuwasaidia watu wa Iran. Hata hivyo, kwa azma thabiti, taifa la Iran limemshinda adui msaliti, kiasi kwamba leo adui hajui namna ya kujinasua kutoka katika mkwamo huu wa kimkakati.”

Taarifa hiyo imebaini wazi kuwa: “Iran itaendelea katika njia ya muqawama na mapambano dhidi ya Shetani Mkubwa na Shetani Mdogo, yaani Marekani na Israel. Lakini je, mwenendo wa baadhi ya serikali za Kiislamu haupingani na maneno ya Mtume Muhammad (SAW), aliyesema: ‘Ikiwa husikii na kuitikia kilio cha Muislamu aliye katika dhiki, basi wewe si Muislamu’? Hii ni imani ya namna gani?”

Larijani amesisitiza kuwa: “Baadhi ya nchi zimekwenda mbali zaidi, zikidai kwamba kwa sababu Iran imelenga kambi za Marekani na maslahi ya Marekani na Israel ndani ya maeneo yao, basi Iran imekuwa adui yao! Je, Iran ikae kimya tu huku Marekani ikianzisha mashambulizi dhidi yake kutoka kambi zilizoko katika nchi zenu? Hivi ni visingizio tu. Katika pambano la leo, upande mmoja wapo Marekani na Israel; na upande mwingine nio taifa la Kiislamu la Iran pamoja na vikosi vya Muqawama. Ninyi mko upande upi?”

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesisitiza kuwa: “Fikirieni mustakabali wa ulimwengu wa Kiislamu. Mnajua kwamba Marekani si mwaminifu kwenu, na Israel ni adui yenu. Tafakarini, hata kwa muda mfupi, juu ya nafsi zenu na mustakabali wa eneo hili. Iran inawatakia kheri na haina nia ya kuwatawala.”

Mwisho wa taarifa hiyo amesema: “Umoja wa Ummah wa Kiislamu, kwa nguvu zake zote, unaweza kuleta na kuhakikisha usalama na uhuru wa mataifa yote.”